MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba jana
alianzisha mchakato wa kuwania urais kupitia muungano wa kambi ya
upinzani nchini unaofahamika kama Ukawa, huku akisema yeye ndiye mtu
pekee anayefaa kupeperusha bendera ya vyama vya upinzani.
Akitangaza azma yake ya kuwania urais baada ya kuchukua fomu jijini
Dar es Salaam, alisema kutokana na kubobea katika masuala ya uchumi,
amefanya tafiti nyingi kuhusu matatizo ya umaskini yanayowakabili
wananchi wakati nchi ina rasilimali nyingi; hivyo anajua mahali pa
kuanzia mara atakapochaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano.
Kama akifanikiwa kutimiza ndoto hiyo, itakuwa historia ya kipekee kwa
kambi ya upinzani nchini, kwani tangu uchaguzi mkuu wa kwanza katika
mfumo wa vyama vingi mwaka 1995, CCM ndiyo inayong’ara na hivyo
kuendelea kuishika dola.
Aidha, katika chaguzi zilizotangulia tangu 1995, Profesa Lipumba
amekuwa akiwania urais mfululizo, lakini kura zake zimekuwa ‘zikipwaya’.
Hii ina maana kwamba, anawania urais kwa mara ya tano.
Jana, akizungumza kwa kujiamini, alisema anaamini kuwa rasilimali za
taifa hili zikisimamiwa vizuri na kupunguza ufisadi na wizi, fedha za
kuiendesha Serikali zipo nyingi na hivyo akasema kuwa iwapo akiteuliwa
na Ukawa na kisha kuchaguliwa kuwa Rais hatakuwa na mswalie mtume na
mafisadi.
Hata hivyo, Profesa Lipumba alisema yuko tayari kumpigia debe mgombea
mwingine wa Ukawa ambaye atasimamishwa na umoja kuwania nafasi hiyo ya
juu ya uongozi wa taifa, iwapo yeye hatapitishwa.
Umoja huo wa kambi ya upinzani uliokusudia kusimamisha mgombea mmoja
wa urais, na pia kuungana mkono kwenye majimbo katika uchaguzi mkuu wa
mwaka huu, unaundwa na CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD.
No comments:
Post a Comment