Butiama. Mtoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Nyerere, Charles Makongoro, ametangaza nia ya kuwania urais, akisema
anaomba kibali kuisaidia CCM iache rushwa, kuparaganyika na atakapoingia
madarakani, ili asiwaangushe Watanzania, anahitaji chama imara kisicho
na shaka kama ilivyo sasa.
Akitangaza nia hiyo nyumbani kwao Mwitongo,
Butiama jana, Makongoro alisema kutokana na CCM “kubakwa na vibaka,”
inawavunja moyo wanachama na inawakatisha tamaa Watanzania, hivyo
inahitaji kiongozi anayewarudishia matumaini.
“Sisi ndiyo wazalendo tunasema mnapotaka kutupora
hiki chama sisi tupo, turudishieni na mnapoturudishia kipitishie kwa
Makongoro Nyerere mna uhakika chama hiki hakipotei siyo kumkabidhi
kibaka,” alisema Makongoro.
Kabla ya kutangaza nia hiyo alisema, “nitangaze
nisitangaze?, Nitangaze nisitangaze,” akajibiwa na watu waliohudhuria
hafla hiyo ‘tangazaaa...’.
Makongoro aliyesema Sh1 milioni za kuchukulia fomu
anazo hivyo haitaji kuchangiwa, alikataa kusoma hotuba iliyoandaliwa
kwa ajili ya kutaja vipaumbele vyake atakapoingia madarakani na
kuwashangaa wenzake waliotangaza nia kwa kutaja vipaumbele, kuwa
wanafanya faulo kwa sababu ilani ya chama haijatoka.
Alisema wametangaziwa na chama kuwa ilani itakuwa
tayari Julai na kwamba hawezi kutoa kipaumbele vyake halafu baadaye
vitofautiane na vitakavyobainishwa na chama ili asije kulaumiwa.
“Nipo hapa kukiri kwamba sehemu kubwa ya tatizo la
CCM ni kutofuata utaratibu, ukiona kuna kazi inaombwa kwa kufuata
utaratibu na wanaoomba hawafuati utaratibu hawa washtukie mapema,
hawafai,” alisema Makongoro na kuongeza:
“Ukiona mtu anayeomba kazi na hafuati utaratibu
huo ilhali akiujua, ujue siku ukimpa kazi biashara ya kwanza akifika
pale ni kufuta utaratibu huo na kuweka wa kwake ili akae mpaka awe
mfalme wa nchi hii, usimpe!”
Makongoro alisema kibaya zaidi viongozi wa CCM
ambao wameshiriki kuweka utaratibu huo ndiyo wanahusika na kwamba,
ingawa kikao chake hakikuwa cha kuwataja kwa majina walioshiriki kuvunja
utaratibu huo lakini hana jinsi lazima awataje.
Aliwataja baadhi ya wagombea waliokwishatangaza
nia ndani ya chama hicho akisema wamekiuka utaratibu kwa kutoa ahadi
wakati ilani ya chama hao haijapitishwa na mkutano mkuu.
“Wewe (anamtaja mgombea) ni mjumbe wa NEC
umeshiriki na unajua kuwa rasimu ya ilani itapitishwa na Mkutano Mkuu wa
CCM, wewe unatangulia kimbelembele, nakuuliza wewe nani?”
Makongoro alimpiga kijembe mgombea mwingine
akisema hana wasiwasi na uadilifu wala uwezo wa kiongozi huyo lakini
hazingatii msamiati wa kung’atuka kwa kuwa amekuwapo ndani ya Serikali
kwa muda mrefu.
No comments:
Post a Comment