Malalamiko makali ya Oxfam kwa kundi la G7
Kikao cha kundi la G7 kinafanyika leo Jumapili katika mji wa Elmau
nchini Ujerumani katika hali ambayo, shirika lisilo la kiserikali la
Oxfam limeonya kuwa, hatua ya nchi zinazounda kundi hilo ya kuendelea
kutumia makaa ya mawe, inashadidisha njaa duniani kiasi kwamba ifikapo
mwaka 2100, jamii ya mwanadamu itakuwa inapata hasara ya karibu dola
bilioni 450 kila mwaka na hasara kubwa itaikumba sekta ya kilimo.
Shirika la habari la Ufaransa limelinukuu shirika hilo likisema jana
Jumamosi kwamba, matumizi ya makaa ya mawe yataongeza umaskini duniani
kwani kinu chochote kile kinachotumia makaa hayo ni sawa na silaha
hatari ya kuangamiza mazingira. Shirika hilo limesema kuwa, matokeo ya
kutumiwa makaa ya mawe ni kuharibu ardhi za kilimo na kupanda bei za
vyakula na hivyo kuongeza idadi ya watu wanaoteseka kwa njaa
ulimwenguni. Shirika hilo limezitaka nchi zote zilizoendelea ziache
kutumia makaa ya mawe na badala yake zitumie nishati jadidika na kwamba
zinapaswa kubadilisha siasa zao haraka kwani tayari madhara ya kutumia
nishati ya makaa ya mawe ni makubwa. Kwa kweli kundi la G7 ambalo
linaundwa na nchi za Canada, Ufaransa, Ujerumani, Uingereza, Italia,
Japan na Marekani ndizo zinazohusika kwa kiwango kikubwa katika uchafuzi
wa mazingira na hali ya hewa. Ni jambo lililo wazi kwamba kuendelea
kupanda kiwango cha joto ardhini kuna athari mbaya zisizofidika kwa
mazingira na pia kwa sekta ya kilimo hasa katika nchi zinazoendelea na
matokeo yake ni kupungua mazao ya kilimo na hivyo kuongezeka idadi ya
watu wanaoteseka kwa njaa. Hali ni mbaya kiasi kwamba Umoja wa Mataifa
umelazimika kuwekeza kwa ajili ya watu maskini katika nchi zinazoendelea
ili kuona watu hao watasaidiwa vipi iwapo mazingira ya nchi zao
yatazidi kuharibiwa. Jambo la kusikitisha ni kuona kuwa, licha ya dunia
nzima kujua hatari kubwa ya kuharibiwa mazingira na hali ya hewa, lakini
nchi zilizoendelea kiviwanda kama vile Marekani hadi leo hii
zinaendelea kukaidi kushirikiana na nchi nyingine duniani katika
jitihada za kuiokoa dunia na janga hilo. Wakati ambapo nchi hizo
zilizoendelea kiviwanda ndizo wachafuaji wakubwa wa mazingira, madhara
ya uchafuzi huo yanazikumba nchi za Asia na Afrika ambazo hazifaidiki na
maendeleo ya viwanda ya madola makubwa bali zinazidi kukandamizwa.
Watetezi wa hali ya hewa duniani wanasisitizia mno suala la kulipwa
fidia nchi zinazoendelea hususan za Afrika kutokana na uchafuzi wa
mazingira unaofanywa na madola yaliyoendelea kiviwanda. Hata hivyo
madola hayo si tu yanadharau miito hiyo, bali hata yanazidisha matumizi
ya mada zinazohatarisha usalama wa dunia nzima kama makaa ya mawe, bila
ya kujali hasara zinazopata nchi zinazoendelea.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment