Kiongozi wa pili kukabidhiwa ‘kifimbo cha uongozi,’ kama kile cha
Nyerere alikuwa ni Rais Jakaya Kikwete aliyepewa rasmi fimbo yake
mwishoni mwa wiki mjini Arusha, wakati wa maadhimisho ya Siku ya
Kimataifa ya Albino Duniani iliyofanyika kitaifa mjini hapa. Kikwete
ndiye aliyekuwa mgeni rasmi.
Kifimbo cha kwanza cha Mwalimu Nyerere kilichongwa mwanzoni kabisa
mwa miaka ya 1960 na mtaalamu wa sanaa za uchoraji, uchongaji na sayansi
za kitamaduni, Athuman Omari Mwariko, ambaye pia ndiye aliyeisanifu
ngao ya taifa pamoja na mwenge wa amani duniani.
“Nilimchongea tena Mwalimu Nyerere Kifimbo cha Pili mnamo mwaka 1985 kipindi kifupi tu kabla hajastaafu rasmi kutoka Ikulu,”
anasema Mwariko na inaonekana pia ameamua kuchonga kifimbo cha tatu na
kumkabidhi Rais Kikwete kabla kiongozi huyo hajang’atuka madarakani
Oktoba mwaka huu.
Katika maisha yake yote, Mwaruko amechonga fimbo nne tu za uongozi
na waliobahatika kuvibeba vifimbo hivyo maalumu hadi sasa ni Baba wa
Taifa, Mwalimu Nyerere, Rais Jakaya Kikwete na hivi karibuni sasa
itakuwa ni Rais Barack Obama wa Marekani.
“Nimekwisha kupeleka ujumbe maalumu kwa Rais Obama pamoja na
Ikulu ya Marekani ili waandae siku na sehemu maalumu ambayo nitakwenda
na kumkabidhi rasmi kiongozi huyo fimbo maalumu ya uongozi,” alisema Mwaruko ambaye pia amekuwa akiishi na kufanya kazi nchini Marekani kwa miaka mingi.
Kuhusu fimbo ya Mwalimu Nyerere, Mwariko anasema; “Kila kiongozi ni sharti awe na fimbo ya kuongozea,”
anaongeza kuwa alimtengenezea Nyerere fimbo yake ya kwanza wakati
akianza uongozi miaka ya 1960 na baadaye kumkabidhi fimbo ya pili wakati
kiongozi huyo akistaafu urais mwaka 1985.
“Mimi ndiye nina siri ya mti uliotumika kuchongea fimbo hizo,” anasema
Mwariko na kuongeza kuwa fimbo zote za Mwalimu zilikuwa za kawaida tu
na wala hazina nguvu za ziada au miujiza kama watu wanavyozusha.
Makazi yake nchini kwa sasa ni katika eneo la Njoro, katikati ya
Pasua na Majengo, wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro, akasema atakuwepo
hadi baada ya uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu.
Mzee Mwariko alizaliwa mwaka 1949 eneo la Mbuyuni wilayani Moshi,
mkoani Kilimanjaro na alihudhuria masomo ya Msingi Handeni, Tanga na
baadae Moshi kabla ya kujiunga na Kings College ya Uganda na baadaye
Chuo Kikuu Cha Makerere nchini humo.
Mafunzo mengine aliyapata katika Chuo cha Sanaa cha Potopoto cha
Congo Brazaville, Chuo cha Lincoln, Uingereza na Chuo Kikuu Cha Havard,
Marekani. Mwariko ndiye mchoraji pekee kutoka Afrika aliyeshinda tuzo
katika mashindano ya nchini Brazil mwaka 1986.
No comments:
Post a Comment