MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John
Magufuli leo anatarajiwa kuchukua fomu ya uteuzi katika Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) ili kusaka wadhamini na kisha kuidhinishwa kuwa mgombea
katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Waziri huyo wa Ujenzi anatarajiwa kuchukua fomu saa sita kamili
mchana, na kwa mujibu wa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu
ya Taifa ya CCM, Nape Nnauye, mgombea huyo atafuatana na mgombea mwenza,
Samia Suluhu Hassan na viongozi waandamizi wa chama hicho tawala. Nape
aliwaambia waandishi wa habari jana katika Ofisi Ndogo ya CCM, Mtaa wa
Lumumba Dar es Salaam kuwa Dk Magufuli na msafara wake, wataondoka
katika ofisi hizo saa tano asubuhi kwenda Ofisi za NEC zilizoko Mtaa wa
Garden katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
“Mgombea Urais wa CCM, Dk John Magufuli atachukua fomu kesho (leo)
saa sita mchana. Msafara wake utaondoka hapa (Ofisi Ndogo) saa tano
kamili na ataambatana na mgombea mwenza na viongozi waandamizi akiwamo
Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, Katibu Mkuu, wajumbe wa Sekretarieti,
Kamati za Siasa za Wilaya na Mkoa wa Dar es Salaam,” alieleza Nape.
Aliongeza kuwa msafara huo, utapitia katika barabara za Morogoro,
Bibi Titi Mohammed na Ohio, na kurudi kwa njia hizo hadi Ofisi Ndogo
Lumumba ambako Dk Magufuli atatoa neno la shukrani kwa wanachama,
mashabiki na wapenzi wa chama hicho kikongwe na tawala nchini, na
Watanzania kwa ujumla.
“Dk Magufuli akishachukua fomu atarejea hapa Ofisi Ndogo na kutoa
neno la shukrani kwa kuzungumza na Watanzania wataokuwapo, wanachama na
mashabiki wetu ifikapo saa saba mchana,” alieleza Nape ambaye mwishoni
mwa wiki aliongoza katika kura za maoni za ubunge katika Jimbo la Mtama
mkoani Lindi.
Dk Magufuli alishinda uteuzi wa kuwa Mgombea Urais wa CCM katika
vikao vyake vilivyofanyika mjini Dodoma mapema mwezi uliopita,
akiwashinda wenzake 38 ambao walikuwa miongoni mwa 42 waliochukua fomu.
Alikuwa miongoni mwa wagombea watano waliopitishwa na Kamati Kuu na
kisha kupigiwa kura na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM akiwa na Dk
Asha-Rose Migiro, Balozi Amina Salum Ali, January Makamba na Bernard
Membe, ambapo yeye, Dk Migiro na Balozi Amina walishinda kwenda kupigiwa
kura katika Mkutano Mkuu.
Katika Mkutano Mkuu Maalumu uliofanyika kwa siku mbili kuanzia Julai
11, mwaka huu, Dk Magufuli aliwashinda wanawake hao wawili na kupewa
jukumu la kupeperusha bendera ya CCM Oktoba 25, dhidi ya vyama vingine.
Historia yake John Pombe Joseph Magufuli alizaliwa tarehe 29 Oktoba
1959 wilayani Chato mkoani Kagera (sasa mkoa mpya wa Geita). Magufuli
alianza elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Chato wilayani Chato
mwaka 1967 na alihitimu mwaka 1974.
Alijiunga na Shule ya Seminari Katoke wilayani Biharamulo, ambako
alisoma kidato cha kwanza na cha pili mwaka 1975 – 1977. Alihamishiwa
Shule ya Sekondari Lake mkoani Mwanza, ambako alisoma kidato cha tatu na
nne mwaka 1977 - 1978.
Masomo ya kidato cha tano na sita aliyapata mkoani Iringa katika
Shule ya Sekondari Mkwawa kati ya mwaka 1979 na 1981. Alirudi Chuo cha
Ualimu Mkwawa kusomea Stashahada ya Elimu ya Sayansi katika masomo ya
Kemia, Hisabati na Elimu.
Alisoma hapo mwaka 1981 – 1982. Baada ya kuhitimu hapo, alianza kazi
ya ualimu katika Shule ya Sekondari Sengerema mkoani Geita, akifundisha
masomo ya Kemia na Hisabati kati ya mwaka 1982 na 1983.
Baadaye alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika kwa mujibu
wa sheria akianzia Makutupora, Dodoma (Julai - Desemba 1983), kisha
kambi ya Makuyuni, Arusha (Januari hadi Machi 1984) na akamalizia kambi
ya Mpwapwa mkoani Dodoma (Machi – Juni 1984).
Mwaka 1985 alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akisomea Shahada ya
Sayansi ya Elimu akibobea kwenye masomo ya Kemia na Hisabati na
alihitimu mwaka 1988. Mwaka 1989 - 1995 alifanya kazi katika kiwanda cha
Nyanza Cooperative Union (Ltd.) akiwa mkemia na wakati huohuo alianza
masomo ya Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Chuo Kikuu cha Salford
nchini Uingereza, kikishirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako
alisoma kati ya mwaka 1991 na 1994.
Magufuli aliendelea na elimu ya juu zaidi kwa maana ya Shahada ya
Uzamivu ya Kemia kuanzia mwaka 2000 hadi 2009, ambayo aliihitimu katika
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuwa mhitimu wa shahada ya udaktari. Dk
Magufuli ana mke na watoto kadhaa.
Dk Magufuli alichaguliwa kuwa mbunge wa Chato mwaka 1995, na
aliposhinda Rais Benjamin Mkapa alimteua kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya
Miundombinu. Katika uchaguzi wa mwaka 2000, Dk Magufuli aligombea na
kushinda kwa mara ya pili.
Rais Mkapa alimteua kuwa Waziri wa Wizara ya Miundombinu . Mwaka 2005
alichaguliwa kuwa mbunge kwa kipindi cha tatu na Rais Jakaya Kikwete
alimteua kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi hadi mwaka
2008, alipohamishiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambayo aliiongoza hadi
mwaka 2010.
Mwaka 2010 alifanikiwa kuchaguliwa kuwa mbunge kwa mara ya nne na
Rais Kikwete alimrudisha katika Wizara ya Ujenzi, ambako yupo hadi hivi
sasa.
No comments:
Post a Comment