Kikwete akubali kuwa balozi wa chanjo Afrika

RAIS mstaafu Jakaya Kikwete amekubali uteuzi wa kuwa Balozi wa Heshima wa kuhamasisha masuala ya afya na kuwataka Wakuu wa Nchi za Afrika kuweka kipaumbele katika upatikanaji wa huduma za afya katika jamii.


Kikwete aliyasema hayo mjini Addis Ababa nchini Ethiopia juzi, wakati akitoa salamu zake baada ya kukubali kuwa Balozi wa Heshima wa ‘Africa United’ kupitia Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Gavi.

United Africa ni mpango uliobuniwa kusaidia uhamasishaji wa masuala ya afya ukiongozwa na Gavi, CAF, Umoja wa Afrika, Benki ya Dunia na CDC Foundation na wameamua kutumia michezo kama nyenzo mojawapo ya kufanya kampeni ya kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa masuala ya afya yanayolikabili bara la Afrika.

Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Jopo la watu mashuhuri la kumshauri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa juu ya namna bora ya kuendeleza na kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu hususani katika afya ya uzazi ya mama na mtoto, alisema upatikanaji wa chanjo utasaidia kuokoa vifo vingi vya watoto Afrika.

Uteuzi huo umekuja huku Rais huyo mstaafu akiteuliwa pia kuwa Mjumbe Maalumu wa AU nchini Libya.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved