Dr. Bana: CCM Iheshimu Mfumo wa vyama Vingi

Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es salaam ambaye pia ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na mambo ya kijamii Dk Benson Bana amesema chama tawala nchini CCM lazima kikubali utamaduni na kanuni za kukubali mfumo wa vingi vya siasa.


Ameyasema hayo alipokuwa akizungumzia suala la upatikanaji wa Meya wa jiji la Dar es salaam ambapo limegubikwa na mambo ya siasa zizizofaa kwa maendeleo ya wananchi na wapenda demokrasia nchini.

''Kauli za mvutano na malumbano ya UKAWA na chama cha mapinduzi havitasaidia wananchi kwanza wanajidhalilisha, kinachotakiwa ni upinzani kutumia busara lakini chama tawala pia watambue kwamba walipokubali mfumo wa vyama vingi lazima wakubali mabadiliko na kuheshimu mfumo wa vyama vingi

"Hakuna sababu ya msingi ya kuwepo malumbano hadi watu wengine wapigwe na wengine kuwekwa rumande kwanza kazi kubwa ya umeya ni kuongoza vikao ingelikuwa tunatafuta mkurugenzi hapo sawa lakini hili wanakosea kwa kweli''-Amesema Dkt. Bana

Meya wa jiji la Dar es salaam ameshindwa kuchaguliwa mara kadhaa pamoja na kuwepo kwa uhalali wa kufanyika uchaguzi huo jambo ambalo limesababisha malumbano makali na kushikiliwa kwa wabunge wawili wa Chadema Saed Kubenea na Halima Mdee.
==

CHADEMA Kususia ziara na Vikao vya Maendeleo Dar es Salaam


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesusia ziara ya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika manispaa za Temeke, Kinondoni na Ilala na kuthibitisha kutoshiriki katika kikao cha bodi ya barabara kinachotarajiwa kufanyika leo kwa kile wanachodai kushinikiza kuachiwa kwa madiwani na mbunge ambao wanaeshikiliwa na jeshi la polisi.

Akielezsea hatua hiyo jana, Meya wa Manispaa ya Kinondoni Boniface Jacob alisema kuwa hawaoni sababu ya kuendelea na vikao mbalimbali vya jiji wakati hawajui hatma ya wenzao ambao mpaka sasa wanashikiliwa na polisi na wengine wanaitwa kufika kituoni hapo kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kusababisha fujo katika zoezi la uchaguzi wa meya wa Jiji la Dar es Salaam.

Kikao kikubwa cha kujadili mipango ya maendeleo ya jiji la Dar es Salaam kinatarajiwa kufanyika leo  ambapo mada kuu itakuwa ni ujenzi wa barabara katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.

Polisi Wafanya Upekuzi Nyumbani Kwa Halima Mdee


Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam jana lilifanya upekuzi mkubwa katika nyumba ya Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) baada ya kumtilia shaka kuwa na nyaraka muhimu za vikao vya uchaguzi wa Meya wa Jiji hilo.
Kikosi cha jeshi hilo kilifika katika nyumba ya mbunge huyo majira ya saa tisa alasiri na kufanya mazungumzo na Mwanasheria wake, John Mallya ambapo baada ya kukamilisha taratibu za kisheria walianza zoezi la upekuzi uliochukua zaidi ya saa moja.
Kiongozi wa kikosi hicho cha Polisi, aliwaambia waandishi wa habari kuwa walilazimika kufanya upekuzi katika nyumba hiyo baada ya kusadikika kuwa wakati wa vurugu zilizotokea katika ukumbi wa Karimjee jijini humo wikendi iliyopita kufuatia kuahirishwa kwa uchaguzi wa Meya wa Jiji, Mdee aliondoka na faili muhimu lenye madokezo yanayohusu uchaguzi huo.

Hata hivyo, baada ya kukamilisha upekuzi huo, Polisi walijiridhisha kuwa hakukuwa na nyaraka hizo ndani ya nyumba hiyo wala kitu chochote ambacho wangekitilia shaka licha ya kukuta nyaraka nyingi za mbunge huyo. Hivyo, walitoa cheti maalum cha kuthibitisha kuwa hakuwa na nyaraka zozote kinyume cha sheria.
“Wamekagua nyaraka zote. Madai yao ni kuwa Halima alimpora au alichukua nyaraka za kiongozi wa Jiji, lakini wamekuta hakuna jambo lolote ambalo linatiliwa shaka. Na wametoa Certificate inayoonesha kwamba hakuna chochote ambacho kimechukuliwa,” alisema Mwanasheria wa Mbunge huyo, John Mallya.

Mdee alishikiliwa na Polisi na kulala rumande juzi kutokana na tuhuma za kushiriki katika vurugu zilizotokea katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, Jumamosi, Februari 27.
Wengine wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi ni Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara.

Wauguzi sita Temeke wasimamishwa Kazi kwa kuuza gloves


Naibu Waziri wa Afya, Dk Hamis Kigwangalla amewasimamishwa kazi wauguzi sita katika hospitali  ya  Temeke kwa kosa la kuomba rushwa.
Wauguzi waliosimamishwa ni Hadija Salum, Beatrice Temba, Agnes Mwampashe, Elizabeth Mwilawa, Mariam Mohamed na Marion Said, ambao walikuwa zamu katika wodi ya wajawazito wakati wa tukio hilo.

“Nimewasimamisha kazi wauguzi wote waliokuwa zamu jana (juzi) asubuhi, nakuagiza Msajili wa Baraza la Wauguzi uwasimamishe hadi utakapowasafisha kupitia kamati ya msajili,” alisema Dk Kigwangalla.
Mmoja wa wajawazito, Loshan Seif alisema alipowasili juzi asubuhi kwa ajili ya kujifungua, muuguzi mmoja wa zamu alimtaka kulipia Sh5,000 za gloves.
“Siku zote huwa natumia bima lakini jana (juzi) wakaniambia hawatumii, nitoe Sh5,000 za gloves, baadaye niliambiwa natakiwa kuwa na uzi wa mshono, sindano na vingine hivyo kama sina nitoe fedha,” Seif.
Dk Kigwangalla alifanya ziara ya ghafla hospitalini hapo jana saa 9.00 alasiri.

Akizungumza jana alasiri baada ya kufanya ziara ya ghafla Hospitalini hapo na kupata malalamiko hayo kutoka kwa wanawake waliojifungua.
“Mama anaambiwa atoe fedha ya gloves Sh5,000 wakati dukani zinauzwa Sh1,000, nataka liwe fundisho kwa wote wanaotuongezea vifo vya wajawazito kwa tamaa ndogondogo,” alisema Kigwangalla.
Katika ziara hiyo, Dk Kigwangalla alishuhudia ubovu wa vyumba viwili vya upasuaji na kutoa maelekezo kwamba, virekebishwe ndani ya miezi sita.
“Hali ni mbaya ndani ya hizi ‘theater’ zote mbili zifanyiwe ukarabati iwapo itashindikana nitazifunga, lazima ziwe na hadhi yake na nitakuja kukagua,” alisema.

Seleiman Jafo Amemvua Madaraka Meneja wa Mamlaka ya Maji Mji Mdogo wa Kisarawe


Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleiman Jafo amemvua madaraka Meneja wa Mamlaka ya Maji Mji Mdogo wa Kisarawe mkoani Pwani, Listen Materu kwa kile alichodai ameshindwa kusimamia majukumu yake kikamilifu.
Pia, Jafo ameuagiza uongozi wa halmashauri hiyo kuondoa kero zinazolalamikiwa na wananchi hasa idara za ardhi, afya na elimu.
Akisikiliza kero za wapigakura wake juzi, Jafo alisema uchunguzi alioufanya ameubaini kwa miaka mitano iliyopita kuwa baadhi ya watendaji wa vitengo na idara wa halmashauri hiyo walikuwa hawawajibiki kwa makusudi, lengo lao lilikiwa ni kujenga chuki baina ya mbunge na wananchi jambo ambalo limefikia kikomo.

“Kuna watu waligeuza wilaya hii kama shamba la bibi, walikuwa wanatumia mali za umma kwa kufanya ubadhirifu sasa wasiseme kuwa wamesalimika, kama wamehama au wamehamishwa tutawafuata kokote walipo na watawajibishwa kwa mujibu wa sheria,” alisema.
Naibu waziri huyo alisema, kuwavua madaraka na kuwawajibisha watendaji wabovu hakutaishia kwa watumishi waliopo wilayani hapa, bali hata waliofanya ubadhirifu na kuhama au kuhamishiwa maeneo mengine.
Katika kuboresha wilaya hiyo na kuharakisha maendeleo, Jafo alisema ni wajibu wa halmashauri kuhakikisha inatenga maeneo ya ujenzi wa stendi, machinjio na utekelezaji wake ufanyike haraka na kuwataka iwapo watakabiliwa na changamoto za kukwamishwa mpango huo wasisite kuwasiliana naye.

Mbunge wa Kilombero Peter Lijualikali Akamatwa.

Picha ya maktaba
 
Jeshi la Polisi  Mkoani Morogoro, wilayani Kilombero  jana  lilimkamata mbunge wa jimbo la Kilombero (Chadema), Peter Lijualikali kwa madai ya kutaka kuingia katika kikao cha Baraza la Madiwani cha kuapisha na kuchagua mwenyekiti na makamu wake wakati si mpigakura.

Lijualikali alikamatwa nje ya ukumbi wa halmashauri na polisi na kuswekwa rumande katika Kituo Kikuu cha Polisi Wilaya ya Kilombero saa 3.48 asubuhi wakati akiingia kwenye ukumbi huo kama mmoja wa mashuhuda.

Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Kilombero, Shabaan Mikongolo alisema mbunge huyo hakutendewa haki na polisi kwa kuwa alifika eneo hilo kushuhudia matukio ya kuapishwa kwa madiwani.

“Ni kama kuna maelekezo yalitolewa kwa polisi kuwazuia wabunge, Lijualikali na Devotha Minja (Viti Maalumu – Chadema) na mwakilishi wa Katibu Mkuu Chadema kutoingia ukumbini lakini viongozi wengine wa Serikali ngazi ya mkoa na wilaya waliruhusiwa." Alisema Mikongolo

Pia, polisi walizuia waandishi wa habari na kutaka kuwanyang’anya kamera zao kwa sababu ambazo hazikuwekwa bayana.

Katika uchaguzi huo, Diwani wa Sanje (CCM), David Ligazo alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kilombero kwa kura 19 dhidi ya Godfrey Lwena ( CHADEMA)  aliyepata kura 18
©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved