JOTO la urais wa awamu ya tano linazidi kupanda miongoni mwa makada
wa CCM, baada ya baadhi yao kuanza kutangaza nia, na leo Balozi mstaafu
Ali Karume anatarajiwa kufanya hivyo, akilenga kutaka kumrithi Rais
Jakaya Kikwete anayemaliza muda wake Oktoba mwaka huu.
Balozi Karume ambaye ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya
CCM, alisema anakusudia kutangaza nia katika ofisi ya Halmashauri ya
Wilaya ya Kati, Dunga.
Akizungumza na gazeti hili, Karume alisema atajitosa katika
kinyang'anyiro hicho ikiwa ni mara ya pili kufanya hivyo kwa nafasi ya
urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mara ya kwanza ikiwa mwaka
2010.
“Nakusudia kutangaza nia ya kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano kwa
sababu sifa ninazo pamoja na uwezo wa kuongoza Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania,” alisema.
Balozi Karume ni mwanadiplomasia mstaafu ambaye alipata kushika
nafasi za kuwa balozi wa Tanzania katika nchi mbali mbali duniani
zikiwemo Marekani, Ubelgiji, Ujerumani na Italia ambako alistaafia kazi
miaka minne iliyopita.
Wakati Karume akiwatarajiwa kuanika dhamira yake leo, Waziri wa
zamani wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Amina Salum Ali
naye anakusudia kuchukua fomu ya kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano
mjini Dodoma wiki hii.
Akizungumza na gazeti hili wiki iliyopita, alisema ameshawishika
kuchukua fomu ya urais kutokana na nafasi na fursa zilizopo kwa wanawake
kushika nafasi ya uongozi wa ngazi za juu.
Alisema huu sio wakati wa kuwaachia wanaume kufanya kila kitu na
kujiamulia, kwa sababu wanawake wa Tanzania wamewezeshwa na kujengewa
uwezo ambao sasa unatosha kuwafanya kushika nafasi za juu za uongozi.
“Msimamo wangu siku zote naamini kwamba mwanamke anao uwezo mkubwa wa
kushika nafasi za juu za uongozi na ndio maana nimekuwa nikijitokeza
kuwania nafasi hizo kadri inavyowezekana,” alisema.
Mwaka 2000, Amina ilikuwa mwanamke pekee aliyejitokeza kuwania katika
kinyang'anyiro cha urais wa Zanzibar na kuibuka nafasi ya nne kwa
kupambana na Rais mstaafu Abeid Amani Karume na Waziri kiongozi wa
wakati huo Dk Mohammed Gharib Bilal ambaye sasa ni Makamu wa Rais wa
Tanzania.
Mwanasiasa huyo mkongwe ambaye ni Balozi wa Umoja wa Afrika katika
Umoja wa Mataifa (UN), aliwahi kuwa Waziri wa Fedha katika utawala wa
Rais Dk Salmin Amour Juma 'Komandoo’, lakini, amewahi kuwa Waziri wa
Mambo ya Nje, chini ya utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi.
Wanadiplomasia hao, Karume na Amina wanakuwa Wazanzibari pekee hadi
sasa kuonesha nia ya kuingia katika kinyang’anyiro cha urais wa
Tanzania.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar), Vuai Ali Vuai alisema kwa mujibu
wa utaratibu uliowekwa na chama, watu wanaokusudia kuchukua fomu
kuwania nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watalazimika
kwenda Dodoma, yaliko makao makuu ya chama hicho.
No comments:
Post a Comment