MAKADA wawili wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mwigulu Nchemba na
Stephen Wassira wametangaza rasmi nia yao ya kutaka kuwania kupitishwa
na chama hicho, kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwigulu ambaye ni mbunge wa Iramba Mashariki, alitangaza uamuzi wake
huo mjini Dodoma wakati Wassira alitangaza nia hiyo jana jijini Mwanza
mbele ya viongozi, wanachama na waasisi wa TANU na CCM na wananchi.
Hafla hiyo ilifanyika katika Ukumbi wa chuo cha Benki Kuu ya Tanzania
(BOT) Kauli ya Wassira Akihutubia mamia ya wakazi waliofurika katika
maeneo ya chuo hicho, alisema ameamua kutangaza nia yake hiyo kwa sababu
anao uwezo mkubwa wa ndani na nje wa kuongoza nchi.
Pia, alisema amefanya hivyo ili kuvunja baadhi ya minong’ono kutoka
kwa baadhi ya watu, iliyomtaka kutangaza nia hiyo. Aliainisha mambo
makubwa matano, ambayo atayatekeleza endapo atachaguliwa kuwa Rais wa
Tanzania.
“Niwashukuru sana kwa kuacha kazi zenu na mkaja hapa kushuhudia jambo
hili muhimu, kwa zaidi ya mwaka mzima kumekuwepo na minong’ono kutoka
kwa juu ya mimi kuwania urais, leo nimekuja hapa Mwanza kuvunja
minong’ono hiyo na kutangaza wazi kuwa natangaza rasmi kuwania nafasi
hiyo”, alisema.
Alisema ameamua kujitokeza kuwania nafasi ya urais, kwa kuwa yeye ni
mtu sahihi kuongoza nchi. Alisema amefanya kazi kwa karibu na marais
wote wa nchi hii, waliopita tangu awamu ya kwanza hadi ya sasa na kwamba
alikuwa na fursa pekee ya kuwasiliana nao.
Aliongeza kuwa sababu nyingine iliyomsukuma kuwania nafasi hiyo ni
kuwa anaijua vizuri Tanzania kwa kuwa ameshiriki katika siasa za nchi
akiwa angali kijana mdogo wa umri wa miaka 25.
“Mwaka 1970 nikiwa na umri wa miaka 25 nilichaguliwa kuwa Mbunge wa
Jimbo langu la Mwibara wilayani Bunda na nimewatumikia watanzania katika
nyadhifa nyingi za juu kwa miaka 45 iliyopita kwanza kama Mbunge, Mkuu
wa mkoa, Naibu Waziri na baadaye Waziri kamili katika awamu mbalimbali”,
alisema, na kuongeza,
“Baada ya tafakari ya muda mrefu na ya kina kwamba nimeamua ni
sahihi, ni wakati mwafaka na kwa hakika, mimi ndiye mtu sahihi wa
kujitokeza na kuwahudumia watu wa nchi hii “, alisema.
Vipaumbele vyake
Alitaja baadhi ya vipaumbele anavyotarajia kuvitekeleza katika
Serikali yake, endapo watanzania watamchagua kuwa Rais kuwa ni
kuteng’eneza nafasi za ajira kwa vijana, kujenga uwezo wa watanzania
kushiriki kikamilifu katika ukuzaji wa uchumi, kuwekeza katika watu,
ikiwa ni pamoja na kufumua upya mfumo wa elimu ili kuwezesha wafanyakazi
kuwa na ushindani.
Wasira alivitaja vipaumbele vingine atakavyovitekeleza kuwa ni pamoja
na kuwa na ujenzi wa miundombinu inayoendana na mazingira ya Karne 21,
yenye dhamira ya kukuza uchumi wa nchi, kuwezesha ushiriki mpana wa
demokrasia na maendeleo ya kiuchumi sanjari na utekelezaji wa mipango,
Sera na mikakati mbalimbali ya kiserikali.
“Nitaendeleza utawala wa kikatiba, utawala bora na wa sheria, kujenga
uchumi imara wenye kuleta ushindani na Serikali yangu itajengwa katika
misingi iliyowekwa na awamu zilizotangulia, hasa kwa rekodi nzuri ya
mtengamano wa uchumi mpana wa nchi na nitafanya marekebisho makubwa
katika utumishi wa umma ili uendane na wajibu wake wa kuwatumikia
watanzania”, alifafanua Wasira aliongeza kuwa endapo atachaguliwa kuwa
Rais, serikali yake itaimarisha kilimo kwa kuleta mapinduzi makubwa ya
kilimo na uchumi vijijini na kuondokana na kilimo cha jembe la mkono .
“Jembe la mkono sasa tutalipeleka kwenye jumba la makumbusho, hii
itakwenda sanjari na kuwaunganisha wakulima wajiunge katika ushirika ili
waweze kukopeshwa matrekta kwa ajili ya kuimarisha kilimo” alisema.
Aidha, alisema endapo atachaguliwa kuiongoza nchi, Serikali yake
itaanzisha mjadala wa kitaifa wa kupambana na rushwa, ambapo aliweka
bayana kuwa amekuwa ni miongoni mwa viongozi waadilifu waliotumikia nchi
bila ya kupata na kashafa yoyote ile “Tutaanzisha mjadala wa kitaifa wa
kupambana na rushwa, Baba wa taifa aliwahi kusema anayesema atapambana
na rushwa, muangalie machoni kama ana ujasiri wa kupambana na rushwa”,
alisema.
“Mimi sina rekodi ya kuwaibia watanzania, mlisikia katika EPA
sikutajwa, sakata la Escrow nalo sikutajwa, sio kwamba mimi sifanyi kazi
za madaraka, lahasha, Mimi ni Waziri wa Kilimo, ningeweza kuwaibia
mbolea, na nimekaa Ikulu muda mrefu, hakuna biashara pale, mkimchagua
mla rushwa angalieni atauza hadi Ikulu yenu,” alisema Wassir
No comments:
Post a Comment