Ofisi ya fatwa Misri: Hujuma za Daesh Saudia sio Uislamu
Ofisi ya fatwa nchini Misri Darul-Iftaa, imelaani shambulizi la kundi la
kigaidi na kitakfiri la Daesh dhidi ya msikiti wa al-Anuud katika mji
wa Dammam mashariki mwa Saudi Arabia na kukitaja kitendo hicho kuwa,
kinakinzana na mafundisho ya dini Tukufu ya Kiislamu. Taarifa
iliyotolewa na idara hiyo, sanjari na kulaani kitendo hicho cha kigaidi,
imesema kuwa wahusika wa jinai hiyo wanalenga kuibua machafuko na
mauaji makubwa katika nchi za Kiarabu. Watu wanne walipoteza maisha na
wengine 10 kujeruhiwa hapo jana wakati wa sala ya Ijumaa baada ya gaidi
aliyekuwa amebeba mada za miripuko kujilipua karibu na msikiti huo. Hii
ni katika hali ambayo, wiki iliyopita, gaidi mwingine kutoka kundi hilo
la kigaidi na kitakfiri alijiripua katikati ya waumini wa madhehebu ya
Kishia waliokuwa wakisali sala ya Ijumaa katika msikiti wa Qadeeh mkoani
Qatif, na kupelekea makumi ya watu kuuawa na wengine wengi kujerihiwa.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudi Arabia imesema hujuma hiyo ya jana
ilijiri katika eneo la kuegeshea magari la Msikiti wa Imam Hussein (as)
mjini Dammam yapata kilomita 400 kutoka mji mkuu, Riyadh. Miongoni wa
watu waliopoteza maisha ni pamoja na gaidi huyo. Kundi la kigaidi la
Daesh limekiri kuhusika na hujuma hiyo. Ingawa serikali ya Riyadh
imetangaza kutohusika na hujuma hizo za kigaidi, lakini weledi wa mambo
wanasema kuwa yanatekelezwa kwa malengo maalumu na kwa ushirikiano na
viongozi wa serikali. Kufuatia hali hiyo maelfu ya raia wa maeneo ya
mashariki mwa nchi hiyo, wamefanya maandamano makubwa kulaani hujuma
hizo za kigaidi dhidi yao. Katika maandamano yaliyoshuhudiwa katika miji
ya Dammam na Qatif waandamanaji wametaka wahusika wa ugaidi kukamatwa
na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria ili kujibu mashtaka dhidi yao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment