Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika (AfCHPR) katika kikao
chake kilichoanza jijini Arusha, itapitia maombi ya rufani ya mwanamuziki
maarufu nchini, Nguza Viking na John Viking dhidi ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania.
Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na mahakama hiyo
jana, ilieleza kuwa kesi hiyo namba 006/2015 iliyopangwa kusikilizwa
Machi 11 haitasikilizwa katika mahakama ya wazi.
Ni kesi mbili
pekee kati ya 50 zitakazosikilizwa kwenye mahakama ya wazi, ikiwamo
inayomhusu mwanasiasa maarufu wa Rwanda, Victoire Ingabire aliyoifungua
kupinga ukiukwaji wa haki anaofanyiwa na Serikali yake.
Pia, mahakama ilieleza kuwa kikao hicho cha 40 cha kawaida kitakamilika Machi 18 na kutoa uamuzi wa mashauri manne.
Kesi
ya Ingabire inayotarajiwa kuvuta hisia za watu wengi ikizingatiwa
upinzani ambao amekuwa akiuonyesha dhidi ya serikali yake, itasikilizwa
Machi 4.
Katika kesi hiyo, Ingabire pamoja na mambo mengine
anadai haki zake kuvunjwa ambazo zinatajwa kwenye Mkataba wa Mahakama
hiyo Ibara ya 7, 10 na 18 hivyo anaitaka itoe uamuzi.
Pia,
Taasisi ya Action Pour la Protection des Droits de I’Homme (APDH)
inaishtaki Serikali ya Ivory Coast kuvunja mkataba wa Mahakama ya Afrika
na Haki za Binadamu Ibara ya 3 na 17 katika kesi namba 001/2014,
iliyopangwa kusikilizwa Machi 3.
Mahakama hiyo inaundwa na
majaji 11 kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) na inakuwa na
vikao vinne kwa mwaka, kufikia Januari 31 tayari ilikuwa imepokea kesi
74 kati ya hizo 25 imetolewa uamuzi.
Maombi manne yamepelekwa kwa uamuzi zaidi kwenye Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu.
No comments:
Post a Comment