Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk
Willibrod Slaa ameanza ziara ya siku nane barani Ulaya ambako atashiriki
mijadala kuhusu hali ya demokrasia na kukutana na jopo la wataalamu wa
masuala ya uchumi kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika kupata mifumo
sahihi na kujenga taasisi za kusaidia uwajibikaji na kusukuma maendeleo
ya watu.
Katika ziara hiyo ya tatu baada ya mbili
alizofanya Marekani, Dk Slaa anatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo
na viongozi mbalimbali wa Umoja wa Ulaya (EU) kuhusu hali ya demokrasia,
utawala bora na hali ya haki za binadamu nchini hasa kwa kipindi hiki
ambacho Watanzania wanaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Idara ya Mambo
ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa wa chama hicho, Deogratias Munishi
ilisema: “Katika ziara hiyo, viongozi hao wa Ulaya watapata fursa ya
kujadiliana na Dk Slaa hali ya siasa kwa ukanda wa Afrika Mashariki.”
Dk Slaa ambaye aliondoka Jumamosi iliyopita,
ameongozana na Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri wa chama hicho, John
Mrema na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini
Makene, ameanza ziara akiwa ametoka katika mikoa ya Kagera, Mbeya, Rukwa
na Katavi akikagua uandikishaji wapigakura kwenye kwa mfumo wa BVR na
kuhamasisha wananchi wenye sifa kujiandikisha.
Kiongozi huyo ambaye anatajwa kuwania nafasi ya
urais ndani ya Ukawa, anafanya ziara hiyo ukiwa umepita mwezi mmoja na
nusu tangu alipofanya ziara ya pili nchini Marekani.
Aprili 13 mwaka huu, Dk Slaa alianza ziara ya siku tisa Marekani
ambako alishiriki mijadala inayohusu uwekezaji, elimu na uongozi ikiwa
na lengo la kuitangaza Tanzania.
Katika ziara hiyo alifanya mihadhara kwenye vyuo
vikuu vya Purdue, Indianapolis na Marion pamoja na vikao vya mashauriano
na baadhi ya wahadhiri wa vyuo hivyo kwa lengo la kubadilishana uzoefu
juu ya masuala ya kisiasa na maendeleo, kijamii na ushiriki wa Chadema
katika siasa za kimataifa.
Pia, alikutana na viongozi wa taasisi pamoja na
kampuni kubwa za uwekezaji kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika
usimamiaji wa masuala ya uchumi na uwekezaji Afrika na kipekee kwa
Tanzania.
Septemba 21, 2013, Dk Slaa alifanya ziara ya wiki
tatu nchini humo na alitembelea majimbo mawili ambako alizungumza na
Watanzania waishio Marekani na kukutana na viongozi pamoja na kutembelea
vyuo vikuu kadhaa katika majimbo ya North Carolina na Alabama. Dk Slaa
alihutubia katika Chuo Kikuu cha Stamford ambako aliutangaza utalii na
fursa za uwekezaji nchini, akisema Tanzania ni nchi tajiri isiyohitaji
misaada kutoka popote kama haijapatwa na janga.
“Viongozi wengi wa Afrika wanaaminika kwenda Ulaya
na Marekani kuomba misaada. Hii imewajengea taswira kuwa Waafrika wengi
ni maskini na wavivu. Lakini ukweli ni kwamba Afrika ipo katika kipindi
cha mpito kujitegemea kwa kila kitu. Sijaja hapa kuomba kwa sababu nchi
yangu ni tajiri sana,” alisema Dk Slaa na kuongeza: “Chama changu
hakiamini katika misaada. Hiyo ni kwa nchi zenye majanga kama
ilivyotokea kwa Rwanda ambayo sasa inajitegemea. Nchi yetu ina
rasilimali za kutosha. Tunao upungufu wa rasilimali watu pekee,
changamoto kubwa iliyopo ni kuimarisha mfumo wetu wa elimu,” alisema.
No comments:
Post a Comment