RAIS Jakaya Kikwete, amesema mara baada ya kung’atuka madarakani
baadaye mwaka huu, ataanzisha taasisi yake itakayojikita zaidi katika
kushughulikia masuala yanayowagusa watoto, wanawake na maendeleo ya
kilimo.
Aidha, amesema angependa kutumia muda wake mwingi kufanya kazi ya
kuwasaidia Watanzania kuinuka kiuchumi, badala ya majukumu mengine ya
kimataifa, yakiwemo ya usuluhisho wa migogoro.
Aliyasema hayo hivi karibuni mjini The Hague, Uholanzi katika mkutano
wake na Watanzania waishio nchini humo uliokuwa na lengo la kuzungumza
nao na pia kutumia fursa hiyo kuwaaga rasmi kwa kuwa muda wake wa kuwa
madarakani utaofikia ukomo kwa mujibu wa Katiba Oktoba mwaka huu.
Akiwa katika Hoteli ya Crownie Plaza, alisema anakusudia kuanzisha
taasisi itakayosaidia makundi mbalimbali, hasa watoto na wanawake na pia
kundi la wakulima ambao kutokana na wingi wa karibu asilimia 80 ya
Watanzania wote, wakiinuliwa watakuwa na nafasi kubwa ya kuongeza kasi
ya ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Rais Kikwete aliyekuwa katika siku ya pili ya ziara yake Uholanzi,
baada ya kuwa amefanya hivyo Finland na Sweden, alilazimika kuyasema
hayo muda mfupi baada ya umoja wa Watanzania hao kumzawadia begi la
kubeba makabrasha, huku wakisema wanaamini baada ya muda wake wa uongozi
kwisha, atakabidhiwa majukumu mengi ya kimataifa kutokana na heshima
kubwa aliyojijengea duniani.
Walitolea mfano kukabidhiwa jukumu la kusuluhisha migogoro ya
kisiasa, ikiwemo ya Kenya, kuwa ni uthibitisho wa kuaminiwa kwake na
jumuiya ya kimataifa.
Alikabidhiwa pia ngao maalumu ya ushupavu katika uongozi, na kitenge
kwa ajili ya mke wa Rais, Mama Salma, lakini akizungumzia zawadi hizo,
alishukuru na kusema hilo la jukumu la kusuluhisha migogoro ya kimataifa
si kipaumbele chake, kwani anafikiria zaidi kuwatumikia Watanzania kwa
mrengo mwingine.
Aidha, alisema mara kadhaa amekuwa akipenda kuwatumikia Watanzania,
ndiyo maana kabla ya kuwa Rais wa Awamu ya Nne wa Tanzania, aliwahi
kupewa heshima ya kufanya kazi ya kimataifa huko Algiers, Algeria lakini
alikataa.
“Niwe muwazi, hayo ya kimataifa nisingependa kuyafikiria sana, lakini
baada ya kustaafu nafikiria kuanzisha Foundation (Mfuko) utakaojikita
kukabiliana na madhila yanayowakuta watoto, wanawake na wakulima…hiyo
ndiyo kiu yangu kwa sababu makundi haya yanahitaji msaada kweli kweli…,”
alisema.
Kiu ya Rais Kikwete ya kujikita katika kilimo ilionekana dhahiri
katika vikao mbalimbali vya kazi katika ziara yake, kwani alihimiza nchi
wahisani kuiamini Tanzania na kuimiminia misaada, hasa yenye lengo la
kuinua kilimo kwa kuwa misaada yao siku zote inatumika vizuri.
Waziri Koenders aliahidi Serikali ya Uholanzi kuendelea kuisaidia
Tanzania, huku akisisitiza italifanyia kazi ombi la Rais Kikwete katika
kukuza Kilimo nchini Tanzania.
Hata alipokutana na Mfalme Willem-Alexander na pia Waziri Mkuu, Mark
Rute, Rais Kikwete aliendelea kutoa shukrani kwa misaada ya maendeleo na
kuitaka Uholanzi kuendelea kuisaidia Tanzania.
Katika sekta ya kilimo, Uholanzi moja ya nchi ndogo kijiografia,
lakini zilizopiga hatua kubwa kiuchumi, inatamba katika kilimo ikiwa ya
pili kwa uzalishaji wa mazao ya chakula duniani, aidha ndiyo inayotoa
theluthi moja ya bidhaa za mboga katika nchi za Jumuiya ya Ulaya.
No comments:
Post a Comment