WAZIRI wa Sheria na Katiba, Dk Asha-Rose Migiro leo anatarajia
kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuteuliwa kuwania nafasi ya urais
kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Aidha, taarifa zilizozagaa kwenye mitandao ya kijamii, kuwa Waziri wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein kuwa atachukua
fomu si za kweli kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya CCM.
Migiro, ambaye atachukua fomu kwenye makao makuu wa CCM mjini hapa
saa tisa mchana, atakuwa mwanamke wa nne kuchukua fomu za kuwania nafasi
hiyo ya juu ya kuiongoza nchi kwa miaka mitano ijayo.
Akiwa ametanguliwa na wanawake wengine Balozi wa Umoja wa Afrika (AU)
nchini Marekani, Amina Salum Ally, aliyekuwa Mbunge wa Iringa na pia
alishakuwa Naibu Waziri wa Fedha, Monica Mbega, Mkurugenzi Mkuu wa
Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk Mwele Malecela.
Migiro aliyewahi kushika wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa (UN), atatanguliwa na kada wa CCM, Salum Marupu ambaye
anatarajia kuchukuwa fomu za kuwania nafasi ya urais saa nne asubuhi.
Aidha, katika siku ya leo, Waziri wa Uchukuzi na Mbunge wa Jimbo la
Urambo Mashariki, Samuel Sitta anatarajia kurudisha fomu yake baada ya
kupata wadhamini katika mikoa 15 ya Bara na Zanzibar.
No comments:
Post a Comment