HATIMAYE Serikali imekata mzizi wa fitina kwa kumaliza mgogoro wa
ardhi wa muda mrefu uliokuwepo baina ya wakazi wa Chasimba na mwekezaji
wa kiwanda cha saruji cha Wazo Hill, kwa kuirudisha ardhi hiyo kwa
wananchi.
Hata hivyo, ardhi hiyo imerudishwa kwa wananchi hao ikiwa na masharti
ambayo ni pamoja na kuachana na shughuli za uchimbaji wa chokaa, kokoto
na mawe kutokana na eneo hilo lilipo kata ya Bunju na Wazo kubadilishwa
matumizi na kuwa eneo la makazi kutoka eneo la madini.
Mgogoro huo umemalizwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, William Lukuvi ambaye alikuwa amefuatana na Mkurugenzi wa
Kiwanda hicho, Alfonso Rodrudges na Mbunge wa Kawe Halima Mdee, ambapo
alisema, licha ya ardhi hiyo kurudishwa kwa wananchi kuna mambo ambayo
inabidi wananchi hao wayafuate vinginevyo, mpango huo utasitishwa.
Alisema wananchi hao wa maeneo ya Chasimba, Chatembo na Chachui
walivamia hekta 243 za eneo la kiwanda hicho chenye hekta 922.55 lenye
hati namba 42336, ambapo katika ya hekta hizo wananchi waliokuwa katika
eneo la ekari 213 walikubali kufanyiwa tathmini kwa ajili ya kuondoka
eneo hilo lakini waliokuwa kwenye hekta 30 walikataa na kukimbilia
mahakamani.
“Serikali imekaa na huyu mwekezaji hapa na kufikia makubaliano,
amesema haya mambo yanaweza kubaki kama yalivyo mkitaka na yanaweza
kubadilika kama mkipenda, kuna watu wanataka kuona huu mgogoro
ukiendelea, sasa msiruhusu hilo.
“Uamuzi wa serikali ni kuwa hatoki mtu hapa, ingawa ni lugha ya
kujidai lakini ina masharti yake. Kwanza kichwani mjue kuwa kabla ya leo
nyinyi mlikuwa ni wavamizi, lakini leo tumeamua kuwaondolea hadhi ya
uvamizi na kuwa wamiliki,” alisema Lukuvi.
Hata hivyo alisema hadhi hiyo haiji bure, kwani wapo watu ambao
walikuwepo wakati eneo hilo lilipofanyiwa tathmini kwa mara ya kwanza
mwaka 2012, hivyo serikali itakaa na kukubaliana na watu hao.
Alisema lengo la kukaa na watu hao ambao picha zao zipo na nyaraka za
kulipwa fidia kwa kipindi hicho ni kuepusha watu kutumia nafasi hiyo
kujipenyeza na kupata viwanja katika maeneo hayo ambavyo vitakuwa
vimepimwa.
No comments:
Post a Comment