Kikao cha 135 cha Baraza la
Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi (PGCC) kimemalizika katika mji mkuu wa
Saudi Arabia, Riyadh katika hali ambayo mbali na kuunga mkono
mashambulio ya Saudia nchini Yemen kimelaani pia haki ya Wayemeni ya
kujihami na mashambulio hayo. Katika taarifa yao waliyotoa siku ya
Alkhamisi mwishoni mwa kikao chao hicho, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa
nchi wanachama wa PGCC walilaani mashambulio ya makombora yaliyolenga
baadhi ya maeneo ya mpakani ya Saudia kutokea ardhi ya Yemen na kudai
kwamba ni haki ya Saudia kuchukua hatua za lazima kwa ajili ya kulinda
amani na uthabiti wa ardhi yake pamoja na raia wake. Taarifa hiyo ya
kikao cha Riyadh iliunga mkono pia kikao cha Geneva kitakachozikutanisha
pande hasimu za Yemen ambacho kinatazamiwa kufanyika siku ya Jumapili.
Uungaji mkono wa mawaziri wa nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la
Ghuba ya Uajemi kwa mashambulio ya Saudi Arabia dhidi ya Yemen unamfanya
mtu ajiulize kama hili kweli ni Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya
Uajemi, au Baraza la kutumikia malengo na maslahi ya Saudia? Ukweli ni
kwamba utendaji wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi haukidhi
viwango vya jumuiya na taasisi ya kieneo, kwa sababu PGCC imeonesha kuwa
ni baraza linalotumiwa kuihami na kuiunga mkono klabu ya wafalme, na
liko mbali kabisa na ushughulikiaji wa matakwa na maslahi ya wananchi wa
nchi wanachama. Mfano wa wazi wa suala hili unaonekana katika
uingiliaji kijeshi wa baadhi ya nchi za Kiarabu huko Bahrain. Katika
hali ambayo akthari ya wananchi wa Bahrain wanataka mabadiliko ya
utawala, Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi likiongozwa na utawala
wa Aal Saud limetuma vikosi vyake huko Bahrain ili kuulinda utawala wa
ukoo wa Aal Khalifa na kupambana na wananchi wa nchi hiyo. Nukta
nyengine ni kwamba kila mara utendaji wa PGCC umekuwa ukikidhi na
kudhamini waziwazi malengo na maslahi ya Saudi Arabia. Kwa maneno
mengine, wakati baraza hilo limewahi kukosoa na kulaumu utendaji na
siasa za Qatar, na hata Saudia, Bahrain na Imarati zikaamua kuwaita
nyumbani mabalozi wao waliokuweko Doha, msimamo wa aina hiyo haujawahi
kuchukuliwa katu kuhusiana na Saudia, na sababu yake ni kwamba nchi zote
wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi hazina budi kutii
na kufuata matakwa ya ukoo wa Aal Saud. Na hilo linaonekana dhaahir
shaahir kwenye taarifa ya kikao cha 135 za Mawaziri wa Mambo ya Nje wa
nchi wanachama wa PGCC. Kwani katika hali ambayo mashambulio ya Saudia
dhidi ya Yemen ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa, utawala wa
Aal Saud umefanya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu kwa kuwaua na
kuwajeruhi maelfu ya watu nchini Yemen, hisia za chuki za fikra za
waliowengi katika ulimwengu wa Kiarabu dhidi ya Aal Saud zimeshtadi, na
pia imethibitika kwamba Saudia imeshindwa katika shambulio lake hilo,
lakini taarifa ya mwisho ya kikao cha PGCC imeuunga mkono uovu huo
uliofanywa na utawala wa Kifalme wa Riyadh. Uungaji mkono huo unaonesha
kuwa badala ya PGCC kuwa chombo huru na wanachama wake kutoa mchango wa
maana kwa ajili ya amani na usalama wa Ghuba ya Uajemi, baraza hilo
limegeuka kuwa muhuri tu wa kuidhinisha na kuhalalisha kila hatua ya
upande mmoja inayochukuiwa na utawala wa Aal Saud. Inafaa tuseme kuwa
kama ambavyo zama za mifumo ya tawala za kifalme katika nchi za Kiarabu
zimefikia ukingoni, utendaji wa sasa wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba
ya Uajemi nao pia hauna ufanisi tena, hivyo kuna udharura wa kuangaliwa
na kutathminiwa upya utendaji wa chombo hicho.
No comments:
Post a Comment