Saudia yadondosha mabomu zaidi ya vishada Yemen


Ndege za kivita za Saudi Arabia zimedondosha mabomu zaidi ya vishaada katika hujuma mpya dhidi ya maeneo ya mpakani nchini Yemen mkoani Sa'ada. Katika mashambulio ya jioni ya jana Jumatatu, ndege za Saudia zilidondosha mabomu ya vishada katika maeneo ya makazi ya raia. Mapema mwezi huu shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) liltoa ushahidi unaoonesha kuwa Saudia inatumia mabomu yaliyopigwa marufuku ya vishada katika mashambulio yake dhidi ya wananchi wa Yemen. Utawala wa Aal Saud unakaidi mwito wa kuacha kutumia mabomu hayo ambayo hutumiwa sana na utawala haramu wa Israel dhidi ya raia Wapalestina. Kwengineko Jumatatu hii raia 14 wameuawa katika mkoa wa Lahij nchini Yemen. Watu hao wamepoteza maisha baada ya mabomu ya ndege za Saudia kulenga basi lililokuwa barabarani katika mkoa huo wa kusini magharibi mwa Yemen. Raia wengine wanne wakiwemo watoto wawili wameuawa baada ya ndege za Saudia kushambulia wilaya ya Sahar mkoani Sa'ada. Tangu yalipoanza mashambulio ya kivamizi ya Saudia dhidi ya nchi hiyo Machi 26 mwaka huu, hadi sasa watu wasiopungua 4,000 wameshauawa na wengine zaidi ya 10,000 kujeruhiwa. Aghalabu ya waliouawa ni raia wakiwemo wanawake na watoto. Saudia inaishambulia Yemen kwa madai madarakani harakati ya wananchi ya Ansarullah na kumrejesha kibaraka wake Abdu Rabuh Mansour hadi aliyeko uhamishoni mjini Riyadh.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved