RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema kuwa Zanzibar imekuwa
na uhusiano na ushirikiano mzuri na nchi za Maziwa Makuu, hivyo ipo haja
ya kuimarisha hatua hiyo kwa kuendelea kuutangaza utalii wa Zanzibar
katika nchi hizo.
Dk Shein aliyasema hayo jana, Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya
mazungumzo na Balozi Mteule wa Tanzania nchini Burundi, Rajab Hassan
Gamaha ambaye alifika Ikulu kwa ajili ya kuaga na kupata baraka za rais.
Katika mazungumzo hayo, Dk Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukua juhudi kubwa za kuiimarisha sekta ya
utalii hapa nchini sambamba na kuimarisha vivutio vyake kwa wageni
kutoka nchi mbalimbali duniani zikiwemo nchi za Maziwa Makuu kama vile
Burundi.
Dk Shein alieleza kuwa ni imani yake kubwa kuwa migogoro iliyopo
nchini humo hivi sasa itamalizika kwa msaada mkubwa wa viongozi wa nchi
za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao wamekuwa wakichukua juhudi za
makusudi za kuhakikisha migogoro iliyopo nchini humo inamalizika.
Alisema kuteuliwa kwa Balozi huyo kuiwakilisha Tanzania nchini humo
ni hatua mojawapo ya Tanzania kuendelea kuimarisha uhusiano na
ushirikiano wa kidugu, kidamu na kimipaka na Burundi.
Dk Shein alisema hivi sasa wananchi walio wengi wa Burundi wameanza
kujifunza lugha ya Kiswahili na Zanzibar ni sehemu yenye asili ya lugha
hiyo, hivyo ipo haja ya kuwahamasisha wananchi wa Burundi kuja Zanzibar
kujifunza lugha hiyo kwenye Chuo chake Kikuu cha Taifa cha Zanzibar
(SUZA).
Aidha, Dk Shein alitumia fursa hiyo kumueleza Balozi Gamaha kuwa
wakati ukifika Zanzibar itafanya uchaguzi wake ulio huru na haki huku
akieleza matumaini yake kuwa viongozi wa vyama vya siasa watafuata
matakwa ya Serikali katika kusimamia amani na utulivu.
No comments:
Post a Comment