Raisi wa Simba Evance Aveva |
Simba imekuwa bila kocha mkuu tangu kumalizika kwa Ligi Kuu mwezi uliopita baada ya kushindwana na kocha Goran Kopunovic aliyeifundisha timu hiyo kwa miezi sita kuanzia mwishoni mwa mwaka jana.
Akizungumza na gazeti hili jana, mmoja wa viongozi wa juu wa Simba alisema kocha mpya ameshapatikana na atafuatana na timu Julai mosi kwa kambi itakayowekwa Zanzibar.
“Kambi yetu ya maandalizi itakuwa Zanzibar, itaanza Julai mosi na kocha mpya atafuatana na timu huko,” alisema mtoa habari huyo.
Akizungumzia sababu za suala la kocha mpya kuwa siri kubwa, mtoa habari huyo alisema: “Tunafanya siri kwasababu vyombo vya habari vimetuharibia sana kwa Kim Poulsen”.
“Unajua Poulsen ndio alikuwa awe kocha wetu, lakini alituambia kwamba tusitangaze kwanza mpaka amalizane na timu anayoifundisha, lakini matokeo yake habari zikavuja vyombo vya habari vikaandika na matokeo yake, Kim ikashindikana kuja, hiyo ndio sababu tulimkosa Kim,” alisema.
“Ndio maana sasa hivi jambo hilo tunafanya siri mwenye uwezo wa kulizungumza ni Rais Aveva (Evans) au Hanspope (Zakaria- Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili), wengine hatuhusiwi hata kama kocha tunamfahamu, la muhimu tu jua ameshapatikana na ataanza kazi rasmi tarehe moja,” alisema.
Mwandishi alimtafuta Rais Aveva kwa simu yake ya mkononi, lakini simu iliita bila mafanikio na ndipo alipowasiliana na Hanspope ambaye naye aligoma kuzungumzia suala hilo.
Simba imekuwa chini ya kocha msaidizi Selemani Matola ambaye ndio amekuwa akifanya usajili kwa ajili ya kikosi kitakachoshiriki Ligi Kuu inayotarajiwa kuanza Agosti.
Tayari Simba imeshafanya usajili wa Mrundi Laudit Mavugo, Mussa Mgosi aliyechezea Mtibwa Sugar msimu uliopita, Peter Malyanzi aliyekuwa Mbeya City na kuwaongezea mikataba mipya wachezaji wake Said Ndemla, Hassan Isihaka na Ibrahim Ajibu
No comments:
Post a Comment