TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars inaanza kampeni ya kufuta historia
mbaya ya kufuzu kwa fainali moja tu za Kombe la Mataifa ya Afrika
(Afcon), itakapoivaa Misri kuwania kufuzu fainali za 2017 nchini Gabon.
Tanzania imefuzu kwa fainali za kwanza na za mwisho mwaka 1980 nchini
Nigeria na hadi sasa haijawahi kutia tena mguu katika fainali hizo na
leo itakuwa ugenini Alexandria kuanza kampeni ya kufuta historia hiyo
isiyopendeza.
Taifa Stars na Misri pamoja na Nigeria na Chad wako katika Kundi G la
michuano hiyo ya kwenda Gabon na jana mabingwa wa Afrika 2013, Nigeria
walicheza na Chad katika mechi ya kwanza ya kundi.
Kikosi cha Mart Nooij kinachodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium
Lager kiliwasili salama katika eneo la Borg El Arab jijini Alexandria
tayari kwa mchezo wa leo utakaoanza saa mbili usiku kwa saa za Tanzania.
Taifa Stars iliyokuwa kambini nchini Ethiopia kwa takribani wiki
moja, iliondoka juzi usiku Addis Ababa na kuwasili Cairo saa nane usiku,
kisha kuunganisha kwa usafiri wa basi mpaka Borg El Arab takribani saa
tatu.
Akizungumzia mchezo huo, Nooij alisema anashukuru kikosi kimefika
salama nchini Misri na kipo katika hali nzuri, vijana wana ari na morali
ya hali ya juu, anaamini timu itafanya vizuri katika mchezo huo dhidi
ya wenyeji Misri.
Nooij alisema mchezo huo ni muhimu kwake, na kikosi chake kitacheza
mpira wa kasi na pasi za haraka haraka, huku safu ya ushambuliaji
ikihakikisha inatumia vizuri nafasi itakazozipata.
Aidha, kiungo Amri Kiemba ameungana na wachezaji wengine waliokuwa
kambini Addis Ababa kuchukua nafasi ya Mrisho Ngasa ambaye alishindwa
kuungana na timu kutokana na sababu zilizopo nje ya uwezo wake.
Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Juma Nkamia pia
yuko Alexandria kwa ajili ya kuipa sapoti Taifa Stars katika mchezo huo
muhimu utakaochezwa kwenye Uwanja wa Jeshi la Misri (Borg El Arab)
uliopo takribani kilometa 70 kutoka jijini Alexandria na kilometa 200
kutoka jiji la Cairo.
Lakini katika siku za karibuni, Stars imekuwa haina matokeo mazuri
chini ya Nooij aliyepewa kazi hiyo Aprili mwaka jana, na Watanzania
wengi wamepaza sauti wakitaka kocha huyo Mholanzi atupiwe virago vyake.
Anaingia uwanjani akiwa anashika nafasi ya 127 kwa ubora wa soka
duniani, na anakutana na timu ambayo ina usongo wa kutocheza fainali za
Afrika kwa siku za karibuni kutokana na matatizo ya kisiasa na sasa hilo
wameliweka pembeni na kuanza kujipanga upya ili kurejesha makali yao
katika soka.
No comments:
Post a Comment