Taifa Stars yawafuata Misri leo


https://blogger.googleusercontent.com/img/proxy/AVvXsEiIqXwljNKTy0Idd-03oDO7D706Bo4pKY32go_LbYIC-uhnF7CUXK_uz7j8ZK7nGnsXEogOgDIjbclFT40tLgCkgRbH9FneNhEjMumBs3pGKwB4HeJS2IujfBtLt57-C5bUjM_HHsBgQKlhvro7mwLe-6c_MiqfJSJEjwNMCeAVaH_wCYZZQ-Hk34FUd6ddGo3bF-w=w506-h513
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mart Nooij
  TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premier Lager, leo jioni inatarajiwa kuondoka Addis Ababa nchini Ethiopia kwenda Misri kuanza kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2017 zitakazofanyika Gabon.
Taifa Stars ambayo iliweka kambi ya mazoezi takribani kwa wiki moja jijini Addis Ababa, jana iliendelea na ratiba yake ya mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa ikifanya mazoezi yake asubuhi tu.
Kwa mujibu wa taarifa ya TFF, Kocha Mkuu wa Stars, Mart Nooij alisema anashukuru maendeleo ya kambi ni mazuri timu yake ilifanya mazoezi katika viwanja viwili vizuri Uwanja wa Taifa na Uwanja wa Benki ya Biashara ya Ethiopia.
Nooij alisema amekuwa akiwafundisha wachezaji wake kucheza mpira wa kasi na pasi za haraka haraka, jambo ambalo wachezaji wameonesha kufuata vizuri maelekezo yake na kusema wanamuelewa vizuri.
Akizungumzia mechi dhidi ya Misri keshokutwa, Nooij alisema timu inakwenda kupambana kusaka matokeo mazuri.
“Nafahamu tunaenda kucheza ugenini, nimewaelekeza vijana wangu wanaocheza nafasi ya ushambuliaji kutumia vizuri nafasi tutakazozipata katika mchezo huo,” alisema Mholanzi huyo akizungumzia mechi hiyo ya kwanza ya Kundi G ambalo pia lina timu za Nigeria na Chad.
Aidha, Nooij alisema katika mpira hakuna kinachoshindikana, kambi ya wiki moja Addis Ababa imewasaidia wachezaji kukaa pamoja na kushika maelekezo yake vizuri, hivyo anaamini timu yake itafanya vizuri katika mchezo huo wa kuwania kufuzu kwa fainali za Afcon.
Katika kikosi cha wachezaji wa 22 waliopo kambini jijini Addis Ababa, hakuna mchezaji majeruhi, wachezaji wote wako vizuri kiafya, kifikra na morali ni ya hali ya juu kuelekea kwenye mchezo huo dhidi ya Mafarao.
Taifa Stars inatarajia kuondoka kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia saa tano usiku na kufika Cairo saa nane usiku, kisha kuunganisha safari ya kwenda Alexandria ambako mchezo huo utafanyika.
Mchezo kati ya Misri dhidi ya Tanzania utachezwa kwenye Uwanja wa Borg El Arab kuanzia saa moja jioni kwa saa za Misri sawa na saa mbili kamili usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Waamuzi wa mchezo huo wanatokea nchini Ethiopia ambapo ni Bamlak Tessema Weyesa (mwamuzi wa kati), Kinfe Yilma (mwamuzi msaidizi wa kwanza) na Wolday Hailerague (mwamuzi msaidizi wa pili).

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved