Bongo Star Search yaja kivingine

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgMoyy77ROPXNphAdLughrHoiDL_fKtEED5gYAFfjHZknQrgtjSkstit46wz_5o2xCh8acUZr8m9H_D-e25QkJPxY55-UIBP5Owk1eXZM124Lq4QO1qEfauxodAb1CbeB-HKxfgmBYLSjU/s1600/Madam-Rita-2-Copy.jpg
BAADA ya kupumzika kwa msimu mmoja kufanya maboresho muhimu katika uibuaji wa vipaji vya wanamuziki, Bongo Star Search wamerejea kwa kishindo kwa kuchanganya usakaji wa vipaji na masuala ya mitindo.
Hayo yalisemwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Benchmark Production, Rita Paulsen akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuelezea msimu huu wa BSS wa ‘Jukwaa ni lako kuwa Original’.
“Staili mpya ya kufurahisha kwa msimu huu wa BSS ili kuzidisha hamasa kwa Watanzania na waangaliaji wote wa shindano hili ni pale muziki unapokutana na mitindo,” alisema Paulsen na kuongeza kuwa wabunifu wakubwa watashiriki katika kipindi kwa kuwabunia mavazi yanayovutia na kuendana na kile wanachokiwakilisha.
Mmoja wa wabunifu hao ni Ally Rhemtullah. Pia alisema tofauti na ilivyozoeleka, msimu huu utakuwa na vituo vinne, ambapo kila kituo kitatoa washiriki watano na 15 watatoka Dar es Salaam.
Alitaja vituo hivyo vya kanda kuwa ni Dar es Salaam, Mbeya, Arusha na Mwanza.
Hata hivyo, kupitia mfumo wa mitandao ya kijamii watu wanaotaka kushiriki watapata nafasi ya kuposti muziki wao ambao utaangaliwa na majaji na kama wataenda vyema watashirikishwa katika michuano ya kikanda kupitia vituo.
“Baada ya miaka nane ya mafanikio ya kuibua vipaji vya wanamuziki, Bongo Star Search inawaahidi kuteka tena hisia zenu kwa mwaka huu wa 2015,” alisema Paulsen ambaye alisema mwaka huu donge ni nono kwa mshindi.
Imeelezwa kuwa washiriki wote 50 watakutana Dar es Salaam kwa uchanganuzi na 20 bora wataingia chuoni kwa harakati za mwisho za kumsaka mshindi. Aidha, Paulsen alisema kwamba kwa mwaka huu wadhamini wakubwa wa shindano hilo ni PSI.
Aidha, kampuni ya kusimamia wanamuziki ambayo inamsimamia Nassib Abdul ‘Diamond Platnumz,’ Shaa, Chegge, Madee na Bendi ya Yamoto, Tip Top Connections, itafanya kazi na BSS ya kuwasimamia washiriki watano bora na kuwaratibu washiriki chini ya usimamizi wao.
Tasnia ya filamu Bongo nayo pia itakutana na tasnia ya muziki kupitia Bongo Star Search.
Usaili wa washiriki Mwanza utafanyika Hoteli ya La Kairo, Arusha utafanyikia Triple A Hotel, Mbeya utafanyikia Club Vibes na Dar es Salaam itatangazwa baadaye.
Bongo Star Search itaanza kurushwa Julai 19, mwaka huu na itarushwa hewani kupitia Clouds TV na Star TV.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved