Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira Mhe. Dkt. Injinia Binilith Satano Mahenge akitoa tamko kuhusu wiki ya mzingira kwa waandishi wa habari (hawapo pichani).
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira, Dkt. Binillith
S.Mahenge amesema Tarehe 5 Juni ya kila mwaka watanzania tunaungana na
mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani. Kitaifa
Maadhimisho haya yataadhimishwa katika viwanja vya Tangamano, Mkoani
Tanga.Kimataifa kaulimbiu inayongoza Maadhimisho haya ni : "Ndoto Bilioni Saba. Dunia moja. Tumia Rasilimali kwa Uangalifu". (Seven Billion Dreams. One Planet. Consume with Care).
Ujumbe wa maadhimisho haya, unahimiza matumizi endelevu ya rasilimali zilizopo, ili kukidhi mahitaji ya idadi ya watu inayoongezeka duniani. Hivyo, ni muhimu kuwa na mikakati ya matumizi endelevu ya rasilimalizilizopo kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
Sote inatubidi kuchukua hatua mahususi za kuhifadhi misitu, uoto wa asili, vyanzo vya maji, maziwa, mito na mabwawa na kupanda miti. Aidha, tunahitaji kudhibiti, uchafuzi wa mazingira utokanao na shughuli za viwandani na umwagaji wa kemikali zenye sumu, utupaji wa taka ovyo, uchimbaji holela wa madini, uvuvi haramu, kilimo kisicho endelevu na shughuli za kibinadamu zisizoendelevu.
Tangazo hili limetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa udhamini wa Kampuni ya Simu ya Airtel -Tanzania, katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani, ambayo Kitaifa itafanyika mkoani Tanga kuanzia tarehe 1 hadi 5 Juni, 2015.
No comments:
Post a Comment