Yanga, Azam FC kujazwa mapesa


ZAWADI kwa ajili ya timu zilizoshika nafasi za juu kwenye Ligi Kuu msimu wa mwaka 2014/2015 zinatarajiwa kutolewa leo.
Katika msimu huo, Yanga ndio ilitwaa ubingwa ikifuatiwa na Azam katika nafasi ya pili na Simba ikimaliza ya tatu na Mbeya City ikishika nafasi ya nne. Yanga kwa kutwaa taji hilo itazawadiwa kitita cha Sh milioni 80.4, Azam itapata Sh milioni 40.2, Simba Sh milioni 28.7 na Mbeya City Sh milioni 22.9.
Taarifa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa waandishi wa habari jana ilisema hafla hiyo iliyoandaliwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kwa kushirikiana na wadhamini wa kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom, inatarajiwa kufanyika leo katika ukumbi wa JB Belmonte (Kilimanjaro) uliopo katika jengo la Golden Jubilee Tower (PSPF), mtaa wa Ohio eneo la Posta Mpya jijini Dar es Salaam kuanzia saa 12 jioni.
Taarifa hiyo ilisema mgeni rasmi katika hafla hiyo ya utoaji zawadi kwa wachezaji, makocha, na timu washindi ni Juma Nkamia, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
Mbali na timu hizo zilizoshika nafasi nne za juu, Vodacom pia itatoa zawadi kwa mchezaji bora wa ligi, tuzo inayowania na Mohamed Hussein (Simba SC), Mrisho Ngasa na Saimon Msuva (Yanga).
Aidha, kutakuwa na tuzo ya kipa bora inayowaniwa na makipa Mohamed Yusup (Prisons), Said Mohamed (Mtibwa Sugar), Shaban Kado (Coastal union).
Tuzo ya kocha bora inawaniwa na Goran Kopunovic (Simba SC), Hans Van Der Pluijm (Yanga) na Mbwana Makata - (Prisons).
Kwa upande wa mwamuzi bora, tuzo hiyo inawaniwa na Israel Nkongo, Jonesia Rukyaa na Samwel Mpenzu. Tuzo ya timu yenye nidhamu inawaniwa na Mgambo JKT, Mtibwa Sugar na Simba.
Kwa mujibu wa mkataba wa Vodacom, mfungaji bora atazawadiwa Sh milioni 5.7, sawa na kipa bora na mchezaji bora.
Timu yenye nidhamu itawazwadiwa Sh milioni 17.2, mwamuzi bora atapata Sh milioni 8.6 sawa na kocha bora.
Katika hatua nyingine, mchezaji John Mahundi wa timu ya Coastal Union amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Mei, 2015 na jopo la makocha kufuatia kuwazidi wachezaji wengine 14 aliokuwa akiwania nao nafasi hiyo.
Kwa kuibuka mchezaji bora wa mwezi huo, Mahundi atazawadiwa fedha taslimu Sh milioni moja kutoka kwa wadhamini wa Ligi Kuu.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved