HUKU akikaribia kukabidhi madaraka kwa Rais wa Awamu ya Tano baadaye
mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete amesema moja ya sifa yake na ya chama
tawala, CCM, ni kutekeleza ahadi walizowaahidi Watanzania wakati wa
kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2010.
Amesema ahadi nyingi alizowaahidi wananchi ambazo ni utekelezaji wa
Ilani ya Uchaguzi ya CCM, zimetekelezwa. Aidha, Waziri wa Ujenzi, Dk
John Magufuli alisema utawala wa Rais Kikwete umekuwa na mafanikio
makubwa kwenye sekta ya ujenzi.
Amesema katika kipindi cha miaka 10, serikali imenunua vivuko vipya
15 na kukarabati vivuko saba na kwamba hayo yote yamefanikiwa kwa kuwa
Watanzania walimuamini Rais Kikwete na kumpa nafasi ya kutekeleza ahadi
kwa vitendo. Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, aliyasema
hayo jana mjini hapa wakati akizindua kivuko cha Mv Mafanikio
kinachofanya safari zake kati ya Mtwara na Msangamkuu.
Alisema wakati wa kampeni mwaka 2010, aliwaahidi wananchi wa
Msangamkuu kuwapatia kivuko ambapo ahadi hiyo imetekelezwa. “Hiyo ndio
sifa yangu pamoja na chama chetu, tunapoahidi tunatekeleza kwa vitendo
na leo hii wananchi wa Msangamkuu wameondokewa na kero ya usafiri
waliokuwa wanapata,” alisema.
Alisema kivuko hicho ni fursa nzuri kwa kukuza uchumi wa wananchi na
amewataka waitumie vizuri fursa hiyo. Rais Kikwete alisema wananchi wa
Msangamkuu walikuwa wanapata shida ya usafiri na kwamba walikuwa
wanalazimika kuzunguka umbali wa kilomita 21 hadi kufika Mtwara mjini,
hivyo adha hiyo kwa sasa itakuwa historia.
Kwa upande wake, Dk Magufuli alisema katika kipindi cha miaka 10 ya
utawala wa Rais Kikwete amefanikiwa kununua vivuko vipya 15 na
kukarabati saba ambavyo hivi sasa vinafanya kazi kwenye maeneo
mbalimbali nchini.
Alisema tangu serikali ya awamu ya kwanza mpaka serikali ya awamu ya
tatu, kulikuwa na vivuko 13 na kwamba hivi sasa vipo zaidi ya 28.
“Hatuna budi kukushukuru Mheshimiwa Rais kwa kuboresha huduma mbalimbali
za usafiri, utawala wako umeweza kununua vivuko vipya 15 na kukarabati
saba hilo si jambo dogo, tunakushukuru sana na rais ajae ataendeleza
zaidi ya hapo ulipoishia,” alisema huku akishangiliwa na mamia ya
wananchi waliojitokeza.
Alisema kivuko hicho kimegharimu Sh bilioni 3.3, ambazo zimetolewa na
serikali. Dk Magufuli ambaye ni mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kupitia CCM, alisema wanafunzi na walemavu watavuka bure
katika kivuko hicho na kwamba watu wazima watalipia Sh 300, watoto Sh
100.
Dk Magufuli alisema Rais Kikwete aliahidi barabara kutoka Dar es
Salaam mpaka Mtwara ambayo hivi sasa imekamilika. “Watanzania wana kila
sababu ya kukushukuru Rais Kikwete umewafanyia mambo mengi, wewe ni
kiongozi mwenye upendo, imani na kubwa zaidi umetekeleza kwa vitendo
uliyoahidi,” alisema.
Aidha alitumia fursa hiyo kujitambulisha kwa wananchi waliojitokeza
kwa wingi kuwa ndiye mgombea urais wa CCM. Mtendaji Mkuu wa Wakala wa
Ufundi na Umeme (TEMESA), Marcelin Magessa, alisema mkoa wa Mtwara kuna
vivuko viwili kikiwemo cha Mv Kilambo na Mv Mafanikio.
Alisema kivuko cha Mv Mafanikio kilitengenezwa na mkandarasi wa hapa
nchini na kwamba kilianza kutoa huduma mwaka jana. Alisema kivuko hicho
kina uwezo wa kubeba abiria 100, tani 50 na magari matatu kwa wakati
mmoja.
Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia, alisema wananchi walikuwa
wakipata shida ya usafi ambapo baadhi yao walipoteza maisha kutokana na
kukosa usafiri wa uhakika. Alisema ujenzi wa kivuko hicho unatokana na
juhudi kubwa zilizofanywa na Dk Magufuli na kwamba wananchi wa jimbo
hilo wanampongeza.
Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendegu, alisema kata ya Msangamkuu
ina wakazi zaidi ya 1,200, ambapo kivuko hicho ni mkombozi mkubwa kwa
wakazi hao. Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika, Naibu
Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mussa
Iyombe, wabunge na wananchi ambao walijitokeza kwa wingi.
No comments:
Post a Comment