MGOMBEA urais wa Chadema anayeungwa mkono na vyama vingine vitatu
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa amewapa
pole wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) kwa mshituko wa kuondokewa na
Mwenyekiti wao wa Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba aliyejiuzulu, huku
akiwataka kutovunjika moyo, bali waongeze mshikamano ili dhamira ya
kuingia Ikulu iweze kutimia.
Aidha, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe ameonya kuwa,
hawatamvumilia yeyote atakayeonekana kutaka kukwamisha umoja wao
unaoundwa na vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.
Akizungumza na wananchi waliofika kumpokea alipotembelea ofisi za CUF
Buguruni, Dar es Salaam jana ambako pia alihudhuria kikao cha Baraza
Kuu la CUF, Lowassa aliwapa pole wanaCUF akisema endapo watatetereka,
safari yao ya kuelekea Ikulu itakuwa ngumu.
Alitumia fursa hiyo kuwaomba wafuasi wa CUF kumsindikiza kwa wingi
leo kwenda ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchukua fomu ya
kuwania urais baadaye mwaka huu, huku akisisitiza ana imani ya kushinda.
Awali, mgombea mwenza wa Lowassa, Juma Duni Haji ambaye alijiunga
Chadema hivi karibuni akitokea CUF alikokuwa Makamu wa Mwenyekiti wa
Taifa, alisema endapo wanachama wa vyama vinavyounda Ukawa watakosea
katika kupiga kura zao na kushindwa kuingia madarakani, basi
watalazimika kusubiri miaka 50 ijayo ili kuingia Ikulu.
“Tusipoweza kuingia Ikulu sasa litakuwa kosa kubwa na itatulazimu
kusubiri miaka 50 ijayo ili kuweza kuchukua madaraka. Vijana pekee ndio
watakaoweza kuleta mabadiliko,” alisema Duni.
Akizungumzia shughuli ya kuchukua fomu leo, Lowassa aliwataka
wanachama wa chama hicho kujitokeza kwa wingi kumsindikiza na kusisitiza
kuwa amejiunga na Ukawa ili kutafuta mabadiliko nje ya CCM na kuwa ana
imani ya kushinda kwa asilimia 90.
Lowassa alisema endapo Ukawa itashinda na kuchukua madaraka
wataendesha nchi kwa utulivu na kubadilisha maisha ya Watanzania kwa
kuwaondolea umasikini ambao umekuwa ukipigwa vita tangu mwaka 1962. Naye
Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe alisema kiongozi ndani ya
Ukawa ambaye atakuwa akipingana na malengo yao kutokana na kukosa fursa
binafsi, mtu huyo hafai kuwa katika umoja huo.
Alisema pamoja na umoja huo kukumbwa na misukosuko, bado wamekuwa
wamoja na kutetea hatua ya wao kumteua Lowassa ambaye wiki mbili
zilizopita alikuwa CCM kwa sababu ni Mtanzania. Katibu Mkuu wa CUF,
Maalim Seif Sharif Hamad alisema silaha pekee ya ushindi kwa Ukawa ni
kuwa na umoja, ushirikiano na mshikamano na kuwa ana uhakika Lowassa
atashinda, sambamba na yeye kwa upande wa Zanzibar.
“Lowassa ni rais anayesubiriwa kuapishwa, na Zanzibar kuna mtu
anaitwa Maalim Seif ameshamaliza kazi naye anasubiri kuapishwa,” alisema
na kuongeza kuwa amefarijika kwa Lowassa kutembelea CUF, jambo ambalo
linadhihirisha umoja wao.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Taifa, James Mbatia alisema Ukawa
haitahubiri siasa za chuki ili uchaguzi ufanyike kwa amani na kuwaonya
viongozi wa CCM kuchunga ndimi zao. Kwa upande wa Mwenyekiti wa Taifa wa
Chama cha NLD, Dk Emmanuel Makaidi alisema watakaoiondoa CCM madarakani
ni wananchi wenyewe kwa kujitokeza kupiga kura.
Lowassa leo atachukua fomu ya uteuzi wa urais katika ofisi za Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC), akiambatana na mgombea mwenza Duni. Msafara wa
kumsindikiza Lowassa, utaanzia Makao Makuu ya CUF, Buguruni asubuhi saa
2:00 na kupitia Makao Makuu ya NCCRMageuzi na baadaye kwenda NEC ambapo
saa 5:00 asubuhi mgombea huyo atachukua fomu.
Baada ya kuchukua fomu, Lowassa ambaye alijiuzulu uwaziri mkuu kwa
kashfa ya kuiingiza Serikali katika mkataba wa kufua umeme wa kampuni
feki ya Richmond na baadaye kuchujwa katika kinyang’anyiro cha kuwania
urais kupitia CCM, atakwenda Makao Makuu ya Chadema, Kinondoni.
Wakati huohuo, Emmanuel Ghula anaripoti kuwa Chama cha Wananchi (CUF)
kimechagua kamati ya watu watatu ambao watafanya kazi zilizokuwa
zikifanywa na Mwenyekiti wa chama hicho aliyejiuzulu, Profesa Ibrahim
Lipumba pamoja na makamu wake, Juma Duni Haji.
Walioteuliwa ni Twaha Taslima ambaye atakuwa mwenyekiti wa kamati,
Abubakar Khamis na Severina Mwijage. Kuundwa kwa kamati hiyo kunatokana
na kujiuzulu kwa aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Lipumba
huku makamu mwenyekiti wake kujiunga na Chadema kama mgombea mwenza wa
urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Akitangaza uamuzi wa baraza kuu la uongozi wa taifa wa chama hicho,
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alisema kuwa chama hakiwezi
kukaa kwa kipindi cha miezi sita bila kuwa na mwenyekiti wala makamu
wake, wameamua kuteua kamati ya watu watatu kama ambavyo katiba yao
inawataka.
“Kwa mujibu wa katiba ya chama chetu, hatuwezi kuteua mwenyekiti wala
makamu wake hadi kipindi cha miezi sita na badala yake katiba
inaturuhusu kuteua kamati ya watu watatu watakaofanya kazi ambazo
zilikuwa zinafanywa na viongozi hao wa juu,” alisema Maalim Seif.
No comments:
Post a Comment