KIVUMBI cha Ligi Kuu Tanzania Bara, kinaendelea tena leo kwenye
viwanja vitano tofauti, huku miamba ya soka Yanga na Simba ikirejea tena
kusaka pointi tatu. Yanga ambayo kabla ya mechi ya Jumatano iliyotoka
sare ya mabao 2-2 na Mwadui FC Uwanja wa Kambarage Shinyanga ilikuwa na
pointi 19 sawa na Azam FC ikiongoza ligi hiyo, ilijikuta ikipata matokeo
hayo ambayo yaliwapa majonzi mashabiki wao.
Majonzi hayo yaliongezeka zaidi Alhamisi baada ya Azam kuibuka na
ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya JKT Ruvu Uwanja wa Karume, Dar es Salaam,
hivyo Azam kuipiku Yanga kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 22
ikiiacha Yanga nafasi ya pili na pointi zake 20.
Kutokana na hali hiyo, leo Yanga itashuka Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi
Tabora kuivaa Kagera Sugar, ikiwa na dhamira moja ya kurejea kileleni
mwa msimamo wa ligi hiyo. Kama Yanga ikishinda leo itafikisha pointi 23
na itaombea Azam FC ambayo kesho itacheza na Toto Africans Uwanja wa
Azam Chamazi ipate matokeo mabovu.
Yanga inapewa nafasi ya kushinda leo kutokana na mwenendo mbaya wa
wenyeji wao Kagera Sugar, ambao tangu kuanza msimu huu wameshinda mchezo
mmoja na kupoteza mitano kati ya tisa waliyocheza.
Leo utakuwa mtihani wa pili kwa Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mohammed
Adolf Rishard, tangu akabidhiwe timu akirithi mikoba ya Mbwana Makatta
aliyeachia ngazi kutokana na matokeo mabaya. Ni wazi Kocha Mkuu wa
Yanga, Hans Pluijm naye ataingia uwanjani kuhakikisha vijana wake
wanaibuka na ushindi ili kuwapa furaha mashabiki wao.
Hata hivyo pamoja na mwanzo mbaya wa Kagera Sugar, lakini timu hiyo
inaweza kuzinduka na kufanya maajabu kwa kuifunga Yanga, kwani inakikosi
bora cha wachezaji waliodumu kwa muda mrefu na timu hiyo akiwemo
nahodha wake George Kavila na Paul Ngwai.
Yanga itaingia kwenye mchezo huo ikizidi kujivunia safu yake ya
ushambuliaji inayoongozwa na Mzimbabwe, Donald Ngoma mwenye mabao saba
na Amissi Tambwe ambao wamekuwa wakipambana kuhakikisha timu yao
inafanya vizuri kwa kufunga mabao mengi.
Kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, Simba inawakaribisha Majimaji
ya Songea huku kocha wake Dylan Kerr, akijivunia ushindi wa bao 1-0,
walioupata kwenye mchezo uliopita dhidi ya Coastal Union ya Tanga na
timu hiyo kufikisha pointi 18 na kupanda hadi nafasi ya nne.
Mshambuliaji Hamisi Kiiza amekuwa tegemeo kwa kocha Kerr, katika
upande wa mabao baada ya kufunga bao lake la sita Jumatano iliyopita
ukiwa ni mchezo wake wa kwanza tangu kurejea uwanjani baada ya kukosa
mechi tatu kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya nyama za paja.
Pamoja na kuonesha kiwango cha chini kwenye mchezo uliopita, lakini
Simba wanapewa nafasi ya kushinda mchezo wa leo kutokana na udhaifu wa
wapinzani wao Majimaji waliopo nafasi ya 10 wakiwa na pointi 11.
Rekodi zinaonesha Majimaji imekuwa hatari msimu huu inapocheza
nyumbani uwanja wa Majimaji Songea, lakini mambo huwa tofauti inapokuwa
ugenini na takwimu zinaonesha imepoteza mchezo mmoja nyumbani na
kushinda mitatu, huku ikifungwa michezo mitatu na miwili ikitoka sare.
Mechi nyingine za leo, Mtibwa Sugar inayoshika nafasi ya tatu kwenye
msimamo, itakuwa nyumbani Uwanja wa Manungu kucheza na Mwadui FC ya
Shinyanga na Prisons itakuwa nyumbani Uwanja wa Sokoine kuchuana na
Ndanda FC ya Mtwara na Coastal Union itakuwa Uwanja wa Mkwakwani
ikicheza na Mbeya City.
Maandalizi ya kumwapisha rais mpya yapamba moto
SERIKALI imeendelea kuandaa mazingira ya sehemu itakayotumika kwa
ajili ya kumwapisha Rais mteule wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli.
Maandalizi ya mazingira hayo yanaenda sambamba na mazoezi ya kijeshi kwa
ajili ya gwaride maalumu, litakalofanyika wakati wa kuapishwa kwake
katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
HabariLeo lilifanikiwa kutembelea katika uwanja huo na kujionea jinsi mazoezi hayo yanavyoendelea, ambapo mmoja wa askari jeshi aliyekuwa akilinda eneo hilo alisema kinachoendelea ndani ya uwanja huo ni mazoezi ya kijeshi kwa ajili ya siku hiyo.
“Mazoezi ya kijeshi na gwaride yanaendelea humu ndani, kwa sasa wananchi wa kawaida hawaruhusiwi kuingia, ila siku husika ikifika wataruhusiwa,” alisema mwanajeshi huyo. Dk Magufuli anatarajia kuapishwa Novemba 5, mwaka huu baada ya kukamilika kwa taratibu zote za uchaguzi na kukabidhiwa cheti cha ushindi.
HabariLeo lilifanikiwa kutembelea katika uwanja huo na kujionea jinsi mazoezi hayo yanavyoendelea, ambapo mmoja wa askari jeshi aliyekuwa akilinda eneo hilo alisema kinachoendelea ndani ya uwanja huo ni mazoezi ya kijeshi kwa ajili ya siku hiyo.
“Mazoezi ya kijeshi na gwaride yanaendelea humu ndani, kwa sasa wananchi wa kawaida hawaruhusiwi kuingia, ila siku husika ikifika wataruhusiwa,” alisema mwanajeshi huyo. Dk Magufuli anatarajia kuapishwa Novemba 5, mwaka huu baada ya kukamilika kwa taratibu zote za uchaguzi na kukabidhiwa cheti cha ushindi.
Subscribe to:
Posts (Atom)