Sambamba na sisitizo la viongozi wa serikali ya Afghanistan katika
kukabiliana na magaidi, makamanda wa jeshi wametangaza kusambaratisha
ngome kuu ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh katika wilaya ya
Achin mkoani Nangarhar, mashariki mwa nchi hiyo.
Zaman Waziri, mmoja wa makamanda wa jeshi la Afghanistan sanjari
na kutangaza habari hiyo, amesema kuwa hivi sasa maeneo mengi ya mkoa
huo yako chini ya udhibiti wa askari wa serikali. Fazal Ahmad Shirzad,
kamanda wa polisi katika mkoa wa Nangarhar amesema kuwa, katika
operesheni dhidi ya magaidi wa kundi la Daesh, askari wa serikali
wamewatia hasara kubwa wanachama wa kundi hilo. Aidha kamanda huyo wa
polisi amewataka wakazi wa mji wa Achin waliokuwa wamekimbia makazi yao
ili kuokoa maisha yao, warejee makwao na kuendelea na maisha yao ya
kawaida ingawa pia amewataka washirikiane na maafisa usalama wa seikali
dhidi ya magenge ya kigaidi. Kwa mujibu wa viongozi wa eneo hilo, jeshi
na askari polisi nchini Afghanistan, wamekuwa wakikabiliana na wanachama
wa genge la kigaidi la Daesh kwa kipindi cha miezi minane sasa katika
wilaya ya Achin mkoani Nangarhar, mashariki mwa nchi hiyo. Hivi sasa
operesheni za kukabiliana na wanachama wa genge hilo, zingali
zinaendelea katika kuzisafisha wilaya nne nyingine za mkoa wa Nangarhar
nchini humo. Maafisa wa seikali wametangaza pia kwamba katika operesheni
za kuusafisha mji wa Achin kutoka mikononi mwa genge hilo, askari wa
serikali wamefanikiwa kudhibiti kiasi kikubwa cha silaha na zana za vita
zilizokuwa zikitumiwa na magaidi hao. Kundi la kigaidi na kitakfiri la
Daesh lilikuwa linajaribu kuudhibiti mkoa wa Nangarhar ili kuubadilisha
kuwa ngome yao kuu nchini Afghanistan. Hata hivyo njama hizo zimefeli
baada ya kukabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa jeshi la nchi hiyo. Kwa
mujibu wa baadhi ya duru za usalama, jeshi la Afghanistan lilianzisha
operesheni kali za kuutwaa mji wa Achin kuanzia tarehe 16 ya mwezi huu
wa Februari. Kwa upande wake msemaji wa jeshi la polisi mkoani
Nangarhar, Hazrat Hussain Mashriqwal, amesema kuwa katika operesheni
hiyo magaidi 50 wa Daesh wameangamizwa. Kwa mujibu wa afisa huyo wa
jeshi la polisi, wakazi wa mkoa huo walishirikiana bega kwa bega na
askari dhidi ya matakfiri hayo maarufu kwa kutenda jinai dhidi ya
binaadamu. Hayo yanajiri katika hali ambayo, katika mwendelezo wa
mafanikio ya serikali ya Kabul dhidi ya magaidi, Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Afghanistan imetangaza kuwa, imefanikiwa kumtia mbaroni mmoja
wa makamanda muhimu wa kundi la kigaidi la Taleban katika mkoa wa Ghor.
Gaidi huyo anayeitwa Mawlawi Abdur-Rahman, alinaswa kupitia operesheni
maalumu za askari wa polisi katika viunga vya wilaya ya Firuzkuh mkoani
Ghor, katikati mwa nchi hiyo. Ripoti za awali zinaeleza kuwa, gaidi huyo
alikuwa mratibu wa hujuma za kigaidi katika mkoa huo. Aidha Wizara ya
Mambo ya ndani ya Afghanistan imewasisitizia wananchi kuwa jeshi la
polisi liko macho na kwamba halitaruhusu maadui kuvuruga usalama wao.
Wakati huohuo, wakazi wa miji kadhaa ikiwemo Kabul, mji mkuu wa nchi
hiyo sanjari na kufanya maandamano makubwa ya kulaani mashambulizi ya
kigaidi, wameitaka serikali kukabiliana vikali na kundi la Taleban na
makundi mengine ya kigaidi yanayovuruga usalama wa nchi yao. Washiriki
wa maandamano hayo, sanjari na kuunga mkono vikosi vya usalama vya nchi
hiyo, wametangaza utayarifu wao kwa ajili ya kukabiliana na magenge hayo
ya kigaidi. Ala kulli hal, kusambaratishwa ngome kuu ya kundi la
kigaidi na kitakfiri la Daesh katika wilaya ya Achin mkoani Nangarhar
kunatajwa na weledi wa mambo kuwa hatua moja mbele katika mafanikio
dhidi ya makundi ya kigaidi ambayo hivi sasa yanataka kujizatiti katika
nchi za Asia ya Kusini na Kati.
No comments:
Post a Comment