Mahakama moja nchini Misri imemUhukumu kifungo cha maisha jela
mtoto mmoja wa miaka 4 kwa tuhuma za kufanya mauaji akiwa na umri wa
baina ya mwaka mmoja na miwili.
Kwa mujibu wa toleo la mtandaoni la gazeti la New Vision la nchini
Uganda, Ahmed Mansour Karmi amepatikana na hatia ya mashtaka manne ya
mauaji, manane ya jaribio la mauaji, shitaka moja la wizi wa kutumia
mabavu na jingine la kuwatishia maisha askari na maafisa wa polisi wa
nchi hiyo, yote hayo akidaiwa kufanya kabla ya kutimiza umri wa miaka
miwili. Ahmed ambaye hakuwa kortini wakati wa hukumu hiyo, ni mmoja kati
ya watuhumiwa 115 ambao wamehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa tuhuma
za kuhusika na jinai zilizofanywa nchini Misri mapema mwaka 2014.
Faisal al-Sayd, wakili wa mtoto huyo amesema kuwa jina la mtoto huyo
liliongezwa kwenye orodha ya watuhumiwa kimakosa na kwamba mahakama
haikumkabidhi jaji aliyetoa hukumu hiyo, cheti cha kuzaliwa cha mtoto
huyo, ili kuhakikisha kuwa alizaliwa Septemba mwaka 2012 au la. Wakili
huyo amesema licha ya kukabidhi cheti hicho, lakini mahakama hiyo
iliipeleka kesi hiyo katika mahakama ya kijeshi ambapo mtoto huyo
alihukumiwa pamoja na watuhumiwa wengine 114. Mwanasheria huyo ambaye
alikuwa akizungumza kwa hasira amesema: “Hii inadhihirisha kuwa jaji
hakuisoma wala kuitafakari kesi iliyokuwa mbele yake na huu ni ushahidi
kwamba hakuna haki nchini Misri.” Ni vyema kuashiria hapa kuwa, zaidi ya
wanachama 40,000 wa upinzani wakiwemo wafuasi wa Ikhwanul Muslimin
wanazuiliwa katika mazingira ya kutisha katika korokoro za nchini Misri
pasina na kufanya kosa lolote. Itakumbukwa kuwa, mwezi Julai mwaka 2013
jeshi la Misri likiongozwa na Jenerali Abdul Fattah al-Sisi lilimpindua
Muhammad Morsi, rais wa kwanza kuwahi kuchaguliwa kidemokrasia katika
nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
No comments:
Post a Comment