MWENYEKITI
wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete amesema
hajahusika kufutwa kwa uchaguzi Zanzibar kwa kumpigia simu Mwenyekiti wa
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha.
Aliyasema
hayo juzi mjini Kibaha wakati wa uzinduzi wa jengo la Ofisi ya Chama ya
Kibaha Mjini mkoani Pwani na kusema maneno hayo ni ya uongo, hayana
ukweli wowote na watu hawapaswi kutoa shutuma hizo juu yake.
Rais
huyo wa Awamu ya Nne alisema maneno hayo hayana kichwa wala miguu wala
hajawahi kumpigia simu Jecha kwa ajili ya kuzungumzia masuala ya kufutwa
kwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar kwani tume hiyo inajitegemea.
“Wasitoe
lawama zisizohusika, wapuuzeni sikuwahi kufanya hivyo hata kwa Damian
Lubuva wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania hivyo nashangaa watu
wanavyosema kuwa nimehusika kufutwa uchaguzi huo,” alisema Kikwete.
“Tume
ya Zanzibar ni tume huru na inajitegemea kwani ina mambo yake hata Dk
Ali Mohamed Shein (Rais wa Zanzibar) hana uwezo wa kuingilia na
kuahirisha uchaguzi huo, watu hao wasipake watu matope wasio husika
kwani kila mtu ana nafasi yake,” alifafanua Kikwete.
Alisema
kikubwa kinachotakiwa ni kuwaombea Wazanzibari wafanye uchaguzi wao
mkuu wa marudio kwa amani na utulivu ili wapate viongozi wao wa
kuiongoza Zanzibar na wawaombee wagombea wa CCM washinde.
Aidha,
alisema chama hicho kinapaswa kuwaadhibu watu waliokihujumu chama
wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana kwa kutomwonea mwanachama, bali
watende haki na si kwa kwa uonevu.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, Mwinshehe Mlao alisema
Mbunge wa Kibaha Mjini, Silvestry Koka ameonesha njia ya kiongozi
kutumia fursa kuboresha mazingira ya utendaji kazi Awali, Koka ambaye
ndiye aliyejenga ofisi hiyo yenye thamani ya Sh milioni 100, alisema
aliamua kujitolea kujenga ofisi hiyo kwa lengo la kukisaidia chama
kiendeshe shughuli zake.
Koka
alisema aliamua kujenga kama kumbukumbu kwa wanaKibaha ili iwe
kielelezo cha uongozi wake kama mbunge wa Jimbo hilo kwa ajili ya
kufanya shughuli za chama badala ya kufanyia sehemu zisizo na hadhi yao.
No comments:
Post a Comment