Polisi ,UKAWA Ngoma Nzito........Naibu Katibu Mkuu CUF Nassor Ahmed Mazrui Naye Atakiwa 'Kujisalimisha' Polisi Kwa Mahojiano


Jeshi la Polisi limeendelea na kamatakamata ya wapinzani wa vyama vinavyounda Ukawa katika maeneo mbalimbali likieleza sababu tofauti za kijinai zinazohusishwa na masuala ya kisiasa.

Mpaka sasa wabunge wa upinzani waliokamatwa ni; Halima Mdee (Kawe), Mwita Waitara (Ukonga) na Peter Lijualikali (Kilombero), wote wa Chadema na baadhi ya madiwani wa chama hicho katika Jiji la Dar es Salaam.
Vilevile, imeelezwa kuwa Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea alikuwa anatafutwa kuunguanishwa na wenzake.

Pia, baadhi ya wanasiasa wa CUF Zanzibar wamekamatwa na kuhojiwa kwa madai ya kuwatusi viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ). 
Viongozi wa CUF waliohojiwa na polisi mpaka sasa ni Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi, Omar Ali Shehe na Kiongozi wa Mkakati wa Ushindi, Mohamed Sultan Mugheir ‘Eddy Riyami’ ambaye yuko nje kwa dhamana.  

Mbali na viongozi hao, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui  jana  amepatiwa barua ya wito  na Polisi Zanzibar  ikielezwa kuna mambo yanamhusu.

Hii ni mara ya pili kwa Mazrui kuitwa polisi tangu kufutwa kwa uchaguzi wa Oktoba 25, huku CUF ikidai kuwa huo ni mwendelezo wa mkakati maalumu dhidi ya viongozi wa chama hicho.
Jana, Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa Umma wa CUF, Maalim Hamad Masoud Hamad alidai kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya kisiasa ya kutaka kumkamata kila kiongozi wa juu wa CUF kuelekea uchaguzi wa marudio.

“Kwa viongozi wa CUF hili halishangazi, nahisi ingelikuwa ni hatua ya kushangaza sana iwapo wanaoitwa kuhojiwa na polisi ni viongozi wa vyama vingine.

"Sisi upande wetu hili ni jambo la kawaida mno na watu wasishangae,” alisema.

Mazrui ambaye pia alikuwa Waziri wa Biashara na Uwekezaji, ametakiwa kuripoti Makao Makuu ya Polisi, Ofisi ya Upelelezi Ziwani mjini hapa kesho saa 2.00 asubuhi na kuonana na mkurugenzi wa makosa ya jinai Zanzibar.

Polisi Zanzibar imethibitisha kuwapo wito huo ikisema kuna mambo muhimu yanayomhusu mwanasiasa huyo.

Rufaa ya Babu Seya na Mwanaye Kuanza Kusikilizwa March 11 Mwaka Huu.


Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika (AfCHPR) katika kikao chake kilichoanza jijini Arusha, itapitia maombi ya rufani ya mwanamuziki maarufu nchini, Nguza Viking na John Viking dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na mahakama hiyo jana, ilieleza kuwa kesi hiyo namba 006/2015 iliyopangwa kusikilizwa Machi 11 haitasikilizwa katika mahakama ya wazi.
Ni kesi mbili pekee kati ya 50 zitakazosikilizwa kwenye mahakama ya wazi, ikiwamo inayomhusu mwanasiasa maarufu wa Rwanda, Victoire Ingabire aliyoifungua kupinga ukiukwaji wa haki anaofanyiwa na Serikali yake.

Pia, mahakama ilieleza kuwa kikao hicho cha 40 cha kawaida kitakamilika Machi 18 na kutoa uamuzi wa mashauri manne.
Kesi ya Ingabire inayotarajiwa kuvuta hisia za watu wengi ikizingatiwa upinzani ambao amekuwa akiuonyesha dhidi ya serikali yake, itasikilizwa Machi 4.
Katika kesi hiyo, Ingabire pamoja na mambo mengine anadai haki zake kuvunjwa ambazo zinatajwa kwenye Mkataba wa Mahakama hiyo Ibara ya 7, 10 na 18 hivyo anaitaka itoe uamuzi.

Pia, Taasisi ya Action Pour la Protection des Droits de I’Homme (APDH) inaishtaki Serikali ya Ivory Coast kuvunja mkataba wa Mahakama ya Afrika na Haki za Binadamu Ibara ya 3 na 17 katika kesi namba 001/2014, iliyopangwa kusikilizwa Machi 3.
Mahakama hiyo inaundwa na majaji 11 kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) na inakuwa na vikao vinne kwa mwaka, kufikia Januari 31 tayari ilikuwa imepokea kesi 74 kati ya hizo 25 imetolewa uamuzi.
Maombi manne yamepelekwa  kwa uamuzi zaidi kwenye Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu.

Polisi Yaua Majambazi Watatu....Baada ya Kupekeliwa Walikutwa na Ujumbe wa Kamanda Suleiman Kova


Watu watatu wanaosadikiwa kujihusisha na vitendo vya kigaidi na ujambazi wameuawa katika majibizano ya risasi na polisi.
Watu hao walikutwa na karatasi yenye ujumbe kwa aliyekuwa Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova ulioandikwa:

“Nasaha kwa Kova, mzee andaa kamati ya mazishi ya vipolisi vyako tukiwamaliza tutakufikia wewe.”

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema jana kuwa tukio hilo, lilitokea Jumamosi iliyopita, eneo la Fire, jijini Arusha wakati mtuhumiwa Athumani Kassim alipokamatwa eneo la Engosheraton akiwa na silaha na aliwataja wenzake.
Kamanda Sabas alisema walipopata taarifa kutoka kwa raia wema walio tilia shaka mwenendo wa mtuhumiwa huyo ambaye alipokamatwa, alikutwa na milipuko, makoti makubwa mawili na kofia ya kuficha uso.
“Baada ya mahojiano, alituambia kuna wenzake wawili anashirikiana nao kufanya uhalifu na tuliweka mtego.

“Saa 5 usiku, askari wetu wakiwa wameambatana na Kassim, walipofika jirani kabisa na nyumba hiyo eneo la Fire, alitoa ishara na wenzake wakaanza kuwashambulia polisi kwa risasi,” alidai kamanda huyo.

Hata hivyo, Sabas alisema polisi waliwazidi nguvu na kuwajeruhi wawili kati yao.
Hata hivyo, magaidi hao walimpiga mwenzao risasi na wao walifariki dunia walipokuwa wakipelekwa hospitali.
Alisema kwenye nyumba waliyokuwa wakiishi, walikuta vitu mbalimbali ikiwamo sare tano za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kofia tano za kuficha nyuso, vazi moja la karate, pikipiki moja iliyobomolewa na imebandikwa namba bandia.
Alivitaja vitu vingine kuwa ni bendera mbili nyeusi zenye maandishi ya Kiarabu zinazotumiwa na makundi ya kigaidi.

Vitu vingine ni kisanduku cha chuma na hati ya kusafiria ya Abrahaman Athuman Kangaa, iliyotolewa Aprili 2, 2013, simu tano za mkononi na kati ya hizo, moja ilitambulika kuwa ni ya marehemu Mary Joseph aliyefariki kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana Februari 20, mwaka huu, eneo la Engosheratoni pamoja na kifurushi cha unga wa baruti na jambia moja.
Miili ya majambazi hao imehifadhiwa katika hospitali ya Mkoa ya Mount Meru kwa ajili ya utambuzi. 

Makamba Aikosoa Serikali ya Kikwete

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba ametofautisha nyakati za utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne iliyoongozwa na Dk. Jakaya Kikwete na zilizopita na huu wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli, huku akiitoa kasoro iliyopita.
Makamba ameeleza kuwa wakati tawala zilizopita, watu walikuwa wakionewa haya na na kujuana kulichukua nafasi tofauti na awamu hii inayochukua hatua stahiki bila kujali.

“Nadhani moja ya changamoto zilizosababisha huko nyuma tusifanikiwe sana katika suala la uwajibikaji, ni hili suala la kuoneana haya. Suala la kujuana kidogo na kusitiriana,” Makamba aliliambia Gazeti la Mwananchi hivi karibuni.
Alisema kuwa utamaduni huo unapoendelea na kuota mizizi, suala la uwajibikaji huwa kikwazo na hatua stahiki dhidi ya watu wanaofanya makosa hushindwa kuchukuliwa.

Makamba ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia katika Serikali ya Awamu ya Nne, alieleza kuwa hatua za utumbuaji majipu zinazochukuliwa hivi sasa dhidi ya wakwepa kodi na watumishi wanaovunja sheria na kutowajibika ni sahihi na kwamba kama kuna mtu anaona anaonewa bado anayo nafasi ya kutafuta haki yake kwenye vyombo vya kisheria.
“Kikubwa tu ambacho mimi ninaamini ni kwamba kunahitajika kujenga utamaduni mpya wa watu kuogopa na kuheshimu wajibu wao, na kwamba hizi kazi si kazi zetu za kudumu. Wakati wote unapofanya makosa basi kuna Mamlaka ya kukuchukulia hatua,” alisema.

Makamba alisisitiza kuwa ni sahihi kuchukua hatua hivi sasa dhidi ya makosa yaliyofanyika katika utawala uliopita, “Kama huko nyuma hakukuwa na utashi wa mfumo wa kuwezesha makosa hayo kubainika, lakini utashi huo upo sasa, basi hatua zichukuliwe.”

Rais Dkt. Magufuli amtumia salamu za Rambirambi, Rais Mstaafu Dkt. Kikwete kufuatia kifo cha Kaka yake

Mzee Seleman Kikwete enzi za uhai wake

EWURA yatangaza kushuka kwa bei ya mafuta

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Felix Ngamlagosi amesema ‘kuanzia tarehe 2 Machi bei za mafuta zimebadilika ikilinganishwa na toleo lililopita la Februari 2016.

Kwa Machi 2016 bei ya rejareja za petroli imepungua Tsh 31 kwa lita sawa na 1.70%, Diesel imepungua Tsh 114 kwa lita sawa na 7.10% na mafuta ya taa yamepungua kwa Tsh 234 kwa lita sawa na 13.75%’

‘kwa kiasi kikubwa, kupungua huku kwa bei za mafuta kwenye soko la ndani kumetokana na kuendelea kushuka kwa bei za mafuta katika soko la dunia






©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved