Bunge la Afrika lataka mapambano dhidi ya ugaidi
Bunge la Afrika limetaka kuzidishwa mapambano zaidi dhidi ya ugaidi
katika nchi za bara hilo. Taarifa iliyotolewa na The Pan-African
Parliament, imezitaka nchi wanachama kutumia nyenzo za kila aina katika
kukabiliana na migogoro ya bara hilo likiwemo wimbi la ugaidi sanjari na
kuifanyia kazi mikataba inayohusiana na suala zima la usalama na amani,
hususan azimio la kidemokrasia na uchaguzi ndani ya nchi za Kiafrika.
Aidha bunge hilo limezitaka pande hasimu katika machafuko ya Burundi,
kuhitimisha mwenendo huo, na badala yake kuupatia ufumbuzi mgogoro huo
ili kuwatumikia wananchi. Limesisitiza kuwa, matatizo hayo yanaweza
kutatuliwa tu kwa njia za amani. Mbali na Burundi The Pan-African
Parliament pia limeitaka jamii ya kimataifa kuingilia kati mgogoro wa
kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram nchini Nigeria, kurejesha
usalama na amani katika maeneo yaliyoathirika na hujuma za kundi hilo na
kumaliza matatizo ya waathirika wa mgogoro huo. Roger Ankodo Dang,
Spika mpya wa Bunge la Afrika ametangaza kuwa, mbali na matatizo ya
ugaidi, bara la Afrika linakabiliwa pia na matatizo mengine yakiwemo
mabadiliko ya hali ya hewa, hali mbaya ya wanawake, afya na masuala ya
elimu, ambayo bila ya kuimarishwa demokrasia ya kweli katika nchi za
bara hilo, itakuwa vigumu kuyatatua. Mwishoni mwa kikao cha bunge hilo
kilichofanyika nchini Afrika Kusini, nchi wanachama zimetakiwa pia
kukabiliana na magendo ya silaha, suala ambalo limetajwa kuwa sababu ya
kuendelea kwa machafuko katika bara hilo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment