Kupuuzwa utambulisho wa Waislamu milioni moja wa Myanmar

                                                                           Licha ya kuwa hatua ya serikali ya Myanmar ya kuwanyima uraia Waislamu wa magharibi mwa nchi hiyo mashuhuri kwa jila la Rohingya, inachukuliwa kuwa sababu kuu ya kuwafanya waikimbie nchi hiyo, lakini kuna haki nyingine za kiraia ambazo Waislamu hao wananyimwa na serikali hiyo. Vyombo vya habari viliripoti siku ya Ijumaa kuwa Waislamu hao wapatao milioni moja na laki tatu hawajawekwa kwenye orodha ya sense ya nchi hiyo kwa jina la Rohingya. Mfuko wa Umoja wa Mataifa unoshughulikia idadi ya watu duniani UNFPA ambao ulisaidia kuhesabu watu nchini Myanmar mwezi Aprili 2014 umesema kuwa zaidi ya Waislamu milioni moja katika jimbo la Rakhine hawakuorodheshwa kwenye sense hiyo kutokana na mivutano ya kikabila. Mabudha walio na misimamo mikali wa Myanmar walionya kwamba hawangeshiriki kwenye zoezi hilo la sense kama Waislamu wangeruhusiwa kutaja utambulisho wao kwenye zoezi hilo. Serikali ya Myanmar inawachukulia Waislamu wanaoishi magharibi mwa nchi hiyo kuwa wahajiri kutoka Bangladesh na kwa msingi huo inawanyima haki zote za kiraia. Hata kikao cha siku moja kilichofanyika hivi karibuni huko Thailand kwa lengo la kutatua tatizo la wahajiri haramu hakikuweza kuzungumzia Waislamu hao wa Myanmar katika taarifa yake ya mwisho. Kikao hicho kilichowashirikisha wawakilishi wa nchi 17 zikiwemo nchi wanachama wa jumuiya ya ASEAN, Marekani, Uswisi na jumbe mbalimbali za kimataifa ukiwemo ujumbe wa UNHCR kilifanyika hivi karibuni huko Thailand kwa lengo la kujadili na kutatua mgogoro wa wakimbizi wa Rohingya na Bangladesh ambao umegeuka na kuwa changamoto kubwa katika eneo hilo. Kikao hicho kimefanyika baada ya Thailand kuwazuia maelfu ya wakimbizi wa Rohingya baharini mwanzoni mwa mwezi huu kwa kisingizio cha kupambana na biashara haramu ya ulanguzi wa binadamu pamoja na magenge ya wafanyabiashara hiyo kusini mwa maji ya nchi hiyo, ambapo wengi walipoteza maisha yao katika hali hiyo. Wengi wa wakimbizi hao ni Waislamu wa Myanmar ambao wamekimbia nchi yao kutokana na ubaguzi, ukandamizaji na mateso wanayofanyiwa na serikali. Waislamu hao wamekuwa wakikimbia nchi yao ya Myanmar tokea mwaka 2012 baada ya Mabudha walio na chuki dhidi ya Waislamu kuanza kuharibu na kuteketeza nyumba zao. Wengi wa Waislamu hao wamekuwa wakiuzwa katika nchi za kigeni na magenge yanayojihusisha na biashara haramu ya binadamu na wengine kulazimika kukimbilia usalama wao katika nchi jirani ambako wanaishi katika mazingira ya kusikitisha kiafya

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved