Naibu Mkuu wa Tume ya
Uchaguzi Burundi ametoroka nchi kabla ya uchaguzi wa bunge na rais huku
mgogoro wa kisiasa ukiendelea kutokota katika nchi hiyo kufuatia uamuzi
wa rais Pierre Nkurunziza kuwania urais kwa muhula wa tatu.
Bi. Spes-Caritas Ndironkeye
anajiunga na jaji mwandamizi pamoja na wakimbizi wengine wa kisiasa
ambao wametoroka Burundi wakihofia maisha yao baada ya kufeli jaribio la
kumpindua Nkurunziza. Jamaa yake Ndironkeye anasema alitoroka akiwa na
binti yake na kuelekea pahala pasipojulikana. Msemaji wa Tume ya
Uchaguzi Burundi inayojulikana kama CENI, Prosper Ntahorwamiye, amesema
tume hiyo imepokea habari hizo lakini akaongeza kuwa hakuna ushahidi
kuhusu Ndironkeye kutoroka nchi. Aidha haijabainika kuwa iwapo
kutokuwepo Ndironkeye kutaathiri uchaguzi wa bunge na serikali za mitaa
uliopangwa kufanyika wiki ijayo au uchaguzi wa rais Juni 26. Leo polisi
wameonekana wakipiga doria katika maeneo mbali mbali ya mji mkuu wa
Burundi, Bujumbura. Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanatazamiwa
kukutana kesho nchini Tanzania kujadili mgogoro wa Burundi.
No comments:
Post a Comment