Takribani watu 2,000 wamepoteza
maisha nchini India kutokana na joto kali ambalo limeikumba nchi hiyo
katika kipindi cha wiki moja iliyopita.
Vifo vingi vimetokea kwenye majimbo ya
kusini ya Andhra Pradesh na Telangana. Kiwango cha joto katika mikoa
hiyo miwili kimefikia nyuzi 47, huku halijoto kwenye mji mkuu wa India
New Delhi ikifikia nyuzi 45. Lakini habari ambazo hazikuthibitishwa
zinasema kuwa kuna uwezekano kuwa kiwango cha joto kimepanda na kufikia
nyuzi 50.
Vifo pia vimeripotiwa katika mkoa wa
magharibi wa Gujarat, ambapo inasemekana kuwa watu wengi waliofariki ni
wale wasio na makazi na vibarua. Mamlaka ya hali ya hewa nchini India
imetabiri kuwa, joto kali litaendelea nchini humo kwa siku mbili zaidi.
Serikali katika mikoa ya kusini
imewataka watu wasitoke nje wakati wa jua kali, na maofisa wa afya
wamependekeza watu wanywe maji kwa wingi kabla ya kutoka nje. Watalaamu
wa masuala ya tiba wamesema kuwa vifo hutokea kutokana na mwili kukosa
maji. Hali kama hii iliwakumba zaidi watu masikini na wasio na makazi
nchini India mwaka 2003 ambapo watu 1,400 walikufa kutokana na joto
kali.
No comments:
Post a Comment