Boko Haram washambulia tena, waua watu 11 Nigeria
Wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram wameua watu
wasiopungua 11 katika shambulio walilofanya mapema leo kwenye viunga vya
mji wa Maiduguri, makao makuu ya jimbo la Borno, lililoko kaskazini
mashariki mwa Nigeria. Hayo ni kwa mujibu wa wakaazi wa eneo hilo pamoja
na duru za usalama za Nigeria. Shambulio hilo limefanywa siku moja tu
baada ya kuapishwa rais mpya wa Nigeria Muhammadu Buhari ambaye ameapa
kulitokomeza kundi hilo la kigaidi na kitakfiri na kuchukua hatua ya
kuhamishia huko Maiduguri makao makuu ya uongozaji wa operesheni za
kijeshi yaliyokuwa mji mkuu Abuja. Milio ya risasi ya silaha za kisasa
ilisikika usiku wa manane wa kuamkia leo katika eneo la kusini magharibi
mwa mji wa Maiduguri. Kwa mujibu wa Mohammed Bunu, mmoja wa wanamgambo
wa kujitolea, kombora la kundi la kigaidi la Boko Haram lililenga nyumba
moja katika eneo la Bulumkutu na kuua watu watano, huku maiti nyengine
sita zikiokotwa katika maeneo mengine tofauti. Shambulio hilo la leo
linafuatia shambulio la miripuko miwili ya mabomu la hapo jana katika
mji wa Tashan Alade ambalo liliua watu wasiopungua saba. Maelfu ya watu
wameuawa na wengine wapatao milioni moja na nusu wamebaki bila makaazi
tangu kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram lilipoanzisha uasi
nchini Nigeria miaka sita iliyopita…/
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment