Mgosi arejea Simba SC


KLABU ya Simba imezidi kujiimarisha baada ya kuwasajili wachezaji wawili, kipa wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), Mohamed Abraham Mohamed na kumrejesha nyumbani mkongwe Mussa Hassan ‘Mgosi’.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hanspoppe, Abraham amesaini mkataba wa miaka miwili wakati Mgosi amesaini mkataba wa mwaka mmoja.
Usajili huo utatimiza jumla ya wachezaji watano baada ya kuwasajili Peter Mwalyanzi, Mohamed Faki na Samil Hajji Nuhu.
Aidha, usajili wa kipa huyo utaongeza idadi ya wale waliopo kufikia wanne, ambao ni Ivo Mapunda, Hussein Sharrif ‘Cassillas’na Peter Manyika.
Kuhusu usajili wa Mgosi, Hanspoppe alisema kuwa amemrejesha tena mchezaji huyo Simba baada ya kuonesha juhudi alipokuwa akiitumikia Mtibwa Sugar msimu uliopita.
Alisema bado ni mchezaji mwenye kiwango kizuri wakaona kuwa si vibaya kumrejesha nyumbani kwani ndiko alikotoka na kufanya vyema misimu iliyopita hivyo kuamini huduma yake inaweza kuwasaidia kujeresha kiwango cha timu.
“Ni kweli tumemsainisha Mgosi, ni mchezaji wetu wa zamani na amekuwa akifanya vizuri, tuna imani naye ndio maana tumempa tena nafasi ya kutusaidia,”alisema.
Mgosi alisajiliwa na Simba mwaka 2005 kutoka Mtibwa Sugar na mwaka 2012 aliuzwa DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo alikocheza kwa misimu miwili na mkataba wake ulipokwisha akasaini timu yake ya zamani Mtibwa Sugar.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 amesajiliwa Simba baada ya kumalizika kwa mkataba wake Mtibwa Sugar hivi karibuni.
Mgosi wakati anahojiwa jana asubuhi na kituo kimoja cha redio, alisema hajasaini isipokuwa amezungumza na kufikia hatua ya kusaini hivyo yuko mbioni kuja Dar es Salaam kumalizana na Simba, kauli ambayo ilionekana kupishana na ile ya Hanspoppe aliyethibitisha kuwa tayari wameshamsajili mchezaji huyo.
Usajili huo wa Hassan unaonesha dhahiri kuwa, Simba wanaifuata Yanga kwa kuwa na wachezaji wenye umri mkubwa, wakati sera yao ilikuwa ni kusajili chipukizi, ambao wataichezea timu hiyo kwa muda mrefu.
Naye mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Collin Frich alisema Mgosi ni mchezaji sahihi kwao na ana uwezo na kiwango chake kipo juu ndio maana wanataka kumrejesha kikosi.
Mgosi akiwa Simba aliwahi kuisaidia timu hiyo kufuzu mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Tusker mwaka 2005 baada ya kuifungia mabao mawili dhidi ya SC Villa ya Uganda akitokea benchi katika uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Katika msimu uliopita, Mgosi alizifunga Simba na Yanga, ambapo katika mabao yake matatu, mawili amevifunga vigogo hivyo.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved