La kukamatwa kwa viongozi FIFA Tanzania tusilipuuze
MOJA ya habari kubwa zilizotawala vyombo vya habari wiki hii, ni sakata la kukamatwa kwa viongozi wa ngazi ya juu wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Viongozi hao walikamatwa wakituhumiwa kushiriki katika suala la ubadhirifu wa fedha za shirikisho hilo kwa njia mbalimbali kama vile kupokea rushwa, kuzungusha fedha chafu na mengineo.
Kukamatwa kwao huko kumezua gumzo karibu kila kona ya dunia, hasa ikizingatiwa kuwa jana ilikuwa ni siku ya Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho hilo ili kumpata rais.
Marais mbalimbali pamoja na viongozi wakubwa wa nchi mbalimbali wameshatoa misimamo yao kuhusu suala hilo, ambapo wapo waliosema kuwa ni sawa wahusika kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria vya nchi zao, huku wengine wakiona ni sawa na kuwa wangeachwa kumaliza suala lao FIFA.
Binafsi naona kuna mengi ya kujifunza katika suala hilo, kwanza ni kuona kwa kiasi gani katika soka, ambavyo rushwa imekithiri pia, suala ambalo ni la kupigwa vita.
Kwa muda mrefu FIFA imekuwa ikituhumiwa kujihusisha na mambo ya rushwa ila imekuwa ikisisitiza kuwa mambo yao yanajadiliwa katika ngazi ya shirikisho hilo.
Hata Sepp Blatter ambaye amekuwa akiliongoza shirikisho hilo kwa miaka mingi, mbali na kukamatwa kwa viongozi hao na kupelekwa kwenye mamlaka za nchi zao kwa maamuzi zaidi ya kisheria, amewatetea na kusema kuwa mamlaka hizo hazitakiwi kuingilia shughuli za soka kwa kuwakamata huku akitaka suala hilo kujadiliwa na wao wenyewe.
Hali kama hiyo imekuwa ikiathiri hata mashirikisho mengine yanayofanya kazi chini ya shirikisho hilo, hiyo ni kwa kuwa wapo watu ambao wamekuwa wakiiba fedha za mashirikisho ya soka kwenye nchi zao na wamekuwa wakijadiliwa katika mashirikisho na hakuna hatua za kisheria zinazochukuliwa.
Hiyo imekuwa ni kikwazo kwa maendeleo ya soka kwa kuwa hutumia hiyo ni kama kivuli cha kujificha dhidi ya ubadhirifu wao na kujikuta wakiathiri maendeleo ya soka.
Kwa kukamatwa tena kwa viongozi wa juu wa FIFA wakituhumiwa kuhusika na rushwa ni dhahiri kuwa kuna rushwa kwenye tasnia hiyo na tena hakuna haja tena ya kuendelea kulindwa eti kwa kusema kuwa masuala ya soka hayajadiliwi mahakamani
Hata kama bado hiyo ndiyo sera, lakini kwa wale wanaokamatwa kuhusika na rushwa au ubadhirifu wowote, basi ni muda umefika wa kuanza kuwakamata sio kuwaacha wakiendelea kufanya ubadhirifu kwa mgongo wa kanuni hiyo ya FIFA ya kuzuia masuala kama hayo kwenda mahakamani.
Yapo makampuni mbalimbali ambayo yamekuwa mstari wa mbele katika kusaidia soka ambayo yanaweza kujitoa kutokana na uzembe wa watu kushindwa kusimamia vema majukumu yao.
Mfano, kampuni kama vile Coca- Cola na Adidas zimetishia kujitoa kwa kuwa hazijapendezeshwa na tuhuma hizo, hapo utaona ni kwa kiasi gani umakini unavyohitajika katika kusimamia kazi kama hizo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment