Sefue ataka simu kuripoti unyanyasaji


KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, ametaka kuwepo kwa namba maalumu ya simu (hotline) itakayotumiwa na makatibu muhtasi kwa ajili ya kupeleka malalamiko dhidi ya unyanyasaji.
Alisema hayo jana mjini hapa wakati akifungua Kongamano la Tano la Kitaifa la Makatibu Muhtasi na Mkutano Mkuu wa Tatu wa Mwaka, unaofanyika mjini hapa chini ya maandalizi ya Chama cha Makatibu Muhtasi Tanzania (TAPSAE).
Balozi Sefue alisema miongoni mwa mambo yanayomuudhi ni unyanyasaji wa kijinsia ndani ya utumishi wa umma na kutaka kuwe na namba hiyo maalumu, ili yeyote atakayenyanyaswa kijinsia awe na mahali pa kupeleka malalamiko yake ili hatua zichukuliwe.
Kwa upande mwingine alikitaka chama hicho kuendeleza jitihada za kuhamasisha wanachama wake kujiendeleza kielimu, kwa kuwa elimu inapoongezeka na ujuzi umekuwa ukiongezeka pia.
Alisema Makatibu Muhtasi ni watumishi wa kutegemewa kuliko watu wanavyofikiri kwa kuwa wamekuwa kiungo muhimu katika ofisi.
Pia alisisitiza umuhimu wa kutunza siri kwani siri zinapovujishwa madhara yake huwa makubwa huku akiahidi Serikali kuangalia upya viwango vya mishahara kwa watumishi hao.
Alishauri vyuo vikuu kuanzisha shahada maalumu ya taaluma hiyo, ili watumishi hao wajiendeleze kwa ngazi ya shahada na ngazi nyingine.
Awali mlezi wa chama hicho, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Dk Mary Nagu alikitaka chama hicho kuendeleza mpango wa kuanzisha Chama cha Kuweka na Kukopa, ili wajiinue kiuchumi na kufanya kazi kwa bidii katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa TAPSEA, Festo Melikio alisema kongamano hilo limehudhuriwa na wanachama 1,005 ambao wamesajiliwa na kuongeza kuwa usajili unaendelea kwa lengo la kupata wanachama 3,000.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved