ACT-Wazalendo yalia na rasilimali nchi



CHAMA cha ACT- Wazalendo kimesema kitaleta sera  mahususi na zenye mapinduzi kuhusu utajiri wa nchi unavyopaswa kuwa na faida kwa wananchi wake.

Hayo yalisemwa na Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe, alipokuwa akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Nkanaredi, mkoani Mtwara.

“Tuna utajiri wa madini, mafuta na gesi. Hapa Mtwara ni kituo kiongozi cha harakati za wananchi kufaidi maliasili zao.  Mliumizwa katika harakati hizo muhimu sana za kuhakikisha kuwa utajiri wa nchi unatumika kwa ajili ya wananchi,” alisema.

Alisema Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imetangaza miswada ya sheria ya kurekebisha sekta ya mafuta na gesi, ambapo wamepeleka miswada hiyo bungeni kwa ajili ya kujadiliwa, huku ikiwa haijawahusisha wananchi.

 “Miswada hii ni miswada muhimu sana kuhusu namna utajiri wa mafuta na gesi ya nchi yetu unapaswa kusimamiwa. Serikali imepeleka miswada hii chini ya hati ya dharura. Kama kuna wadau wakubwa katika sekta ya mafuta na gesi hakuna wadau zaidi ya watu wa Mtwara na Lindi.

“Miswada hii inapelekwa bungeni bila kupata maoni yenu. Haikubaliki, ACT Wazalendo inataka miswada hii iondolewe bungeni ije kwa wananchi ipate maoni na kujadiliwa na Bunge la 11 litakalopatikana baada ya uchaguzi mwaka 2015.

“Muswada wa Mafuta umetungwa bila ya kuzingatia mchakato wa Katiba ya nchi. Rasimu ya Katiba imeondoa suala la mafuta na gesi kwenye orodha ya mambo ya Muungano. Sheria iliyopelekwa bungeni inatamka kuwa sheria hiyo itatumika Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar,” alisema.

Zitto alisema muswada wa usimamizi wa mapato ya mafuta na gesi pia umetamka kutumika pande zote za Muungano kinyume na nia ya kuondoa masuala ya mafuta na gesi  katika orodha ya mambo ya Muungano.

“Ni kichekesho na Serikali kuahidi kwa Wazanzibari kuwa mafuta na gesi si suala la Muungano halafu inatunga sheria za mafuta na gesi za kutumika Zanzibar. Miswada hii haikufikiriwa vizuri na hivyo iondolewe."

Alisema muswada wa mapato ya mafuta na gesi imeandikwa haraka haraka na umeacha kabisa kushughulikia suala la mgawo wa mapato ya mrabaha kwa maeneo yenye utajiri huo.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved