WAZIRI
wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe na Jaji Mkuu Mstaafu,
Augustino Ramadhani, jana walikuwa mkoani Tanga kwa ajili ya kusaka
wadhamini ili waweze kukamilisha sharti la kuomba ridhaa ya kugombea
urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza
wakati akiwashukuru wanachama wa chama hicho waliojitokeza kumdhamini,
Dk Mwakyembe alizungumzia wingi wa wagombea waliojitokeza kuchukua fomu
kwa ajili ya kugombea nafasi ya urais kupitia CCM, akisema umeonyesha
ukuaji wa demokrasia.
“Wenzetu
wanatushangaa na wengine wanahoji kwanini nafasi moja inagombewa na
watu wengi, lakini niwaambie huku ndio kukua kwa demokrasia ndani ya
chama chetu,” alisisitiza Dk. Mwakyembe.
Alisema
yeye kwa upande wake anatamani wagombea urais kupitia CCM wafike 50 ili
chama kiweze kufanya mchujo ambao utakuwa ni wa haki kwa wanachama wote
waliojitokeza katika kinyang’anyiro hicho.
Aidha
Mwakyembe alisema ameamua kugombea nafasi hiyo ili kuleta maendeleo,
kwani anajua vema changamoto na mafanikio yalipatikana katika serikali
ya awamu ya nne.
“Nazijua
fursa zilizopo ambazo zitasaidia kutufikisha kwenye mafanikio na
maendeleo wakati wa awamu ya tano, hivyo sikuona sababu ya kuingia
kinyonge kwenye kinyang’anyiro hicho, kwani mimi ni chaguo sahihi,” alisema.
Kwa
upande wake, Jaji Augustino Ramadhani alisema Tanzania si maskini,
kwani ina rasilimali nyingi ambazo zikitumika vizuri kwa manufaa ya
wananchi zitaleta maendeleo makubwa.
“Ifike
mahali wananchi wazinduke pamoja na viongozi rasilimali zilizopo kama
madini, utalii, mito na mabonde viwekwe kwenye mfuko wa taifa kwa ajili
ya kusaidia watu wote,” alisisitiza.
Aliongeza
kuwa nia ya kugombea nafasi hiyo ni kuhakikisha anawatokomeza kabisa
maadui watatu, ambao nchi inapambana nao toka enzi ya uhuru, ambao ni
umaskini, ujinga na maradhi.
No comments:
Post a Comment