KINAMAMA
kutoka Kata ya Bukundi Wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu, wameandamana
hadi kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Erasto Sima, kushinikiza wapewe miili ya
vijana wao wawili waliouawa na askari Mei 29, mwaka huu.
Vijana
hao Gineu Gidahasi na Gitienga Gidahasi ambao ni ndugu wa familia moja
wanadaiwa kupigwa risasi na askari wa Kampuni ya ulinzi ya Mwiba Holding
kwa madai ya kuingiza mifugo eneo pori la makao ambalo kampuni hiyo
imewekeza.
Kinamama
hao walifika katika ofisi ya Mkuu huyo wa wilaya saa mbili juzi
asubuhi ambapo walilalamikia kitendo cha vijana wao kuuawa na kisha
miili yao kutoonekana na kumwomba Sima kuagiza kupatiwa miili hiyo ili
waweze kuifanyia mazishi na iwapo itashindikana watakwenda kwa Rais
Jakaya Kikwete kuomba msaada huo.
“Tumechoka
na manyanyaso kutoka kwa mwekezaji huyu, kilichotuleta hapa tunahitaji
tupatiwe miili ya vijana wetu tukaifanyie mazishi kwa heshima zote za
kabila letu na iwapo utashindwa kufanya hivyo basi tutakwenda Ikulu
tumuombe Rais Kikwete atusaidie,” alisema Udamulela Gitasori mkazi wa kijiji cha Lukale.
Walisema
hadi sasa zaidi ya vijana sita wameuawa tangu mwaka 2013 kwa madai ya
kuingiza mifugo katika eneo la pori hilo ambalo linapakana na vijiji vya
Mwabagimu, Lukale na Bukundi na hivyo wamekuwa wakiishi kama wakimbizi
ndani ya nchi yao.
Naye
Mbunge wa Jimbo la Meatu, Meshack Opulukwa (Chadema), aliitupia lawama
serikali kwa kushindwa kulipatia ufumbuzi suala la wafugaji kuuawa kwa
kupigwa risasi na askari wa mwekezaji huyo licha ya kupatiwa taarifa na
hivyo alimwomba Sima kusitisha shughuli zinazofanywa na Mwiba hadi hapo
miili hiyo itakapopatikana.
Akijibu
malalamiko hayo kwa kifupi Sima alisema serikali wilayani humo
imeshaanza kulishughulikia suala hilo na tayari wote waliohusika na
mauaji hayo wameshakamatwa.
No comments:
Post a Comment