NAIBU Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba,
anayeomba ridhaa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuteuliwa kugombea urais,
jana alipata idadi kubwa ya wadhamini wanaofikia 3,550 mkoani Ruvuma.
January, ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli, alipata idadi ya wadhamini
hao ambao ni wanachama wenzake wa CCM siku moja tu baada ya kupata idadi
ya wadhamini zaidi ya 700 katika mikoa ya Iringa na Njombe.
Akizungumza katika ofisi za CCM Mkoa wa Ruvuma baada ya kuwasili saa
11:28 asubuhi, huku msafara wake ukiongozwa na pikipiki zaidi 100 na
basi lake lililopambwa kwa picha zake, January alisema amefarijika na
maelfu ya wanachama wenzake waliokwenda kumdhamini.
“Kwa kweli nimefarijika sana na umati mkubwa uliokuja kunidhamini na
kuja kunisikiliza. Leo (jana) hii kwangu ni siku ya historia,” alisema
January.
Kutokana na idadi ya watu kuwa kubwa na kusababisha ukumbi wa CCM
kufurika, ilimlazimu January aombwe na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma,
Oddo Mwisho, kwenda kuzungumza nje ya ofisi hizo.
“Idadi ya watu ni wengi, leo (jana) umepata wadhamini 3,550 na
wengine walitaka kuendelea kukudhamini, lakini ukizungumza tunaomba
utoke nje ya ukumbi ili kila mwana CCM aliyekuja hapa aweze
kukusikiliza,” alisema Oddo.
Baada ya kutoka nje ya ukumbi huo na kuanza kuhutubia maelfu ya
wanachama wa CCM, January aliendelea kuwaomba wana CCM wenzake waliotia
nia ya kuteuliwa kugombea urais kuacha siasa za kuchafuana na badala
yake waonyeshe ukomavu wa kisiasa.
“Tangu nilipotangaza nia na kuanza kuomba wadhamini mikoani
sijamtukana wala kumkebehi mtu kwa sababu nikifanya hivyo nitakuwa
nawapotezea muda nyie mliokuja kunisikiliza, kisha mkiondoka hapa
mtanidharau mimi.
“Tunahitaji kufanya siasa za staha na kistaarabu kwa sababu
akipatikana mgombea mmoja kutoka CCM sisi ndiyo tutakaopanda majukwaani
kumnadi, kwa hiyo tukianza kupakana matope kipindi hiki tutashindwa kula
matapishi yetu wenyewe wakati wa kampeni.
“Kumbukeni kutuangalia sisi tuliotia nia sasa hivi kwa namna
tunavyozungumza sasa hivi au namna tunavyoomba wadhamini mikoani, iwe
kwa kuchafua wengine au kwa kutoa rushwa, ndivyo tutakavyoongoza nchi,”
alisema January.
Alisema kama CCM ikimteua kuwa mgombea kisha akashinda nafasi ya
urais ataongoza nchi kwa weledi mkubwa utakaomfanya kila Mtanzania
ajisikie fahari.
“Mimi nimekulia ndani ya CCM, nina maarifa, uwezo na nikiteuliwa
nitahakikisha tunashinda uchaguzi kwa urahisi na nitaongoza nchi kwa
weledi, sitayumba na matatizo ya wananchi nayajua na majawabu mapya ya
kuyatatua nayajua, kwa kuwa nchi inahitaji kuongozwa kisasa.
“Rais Jakaya Kikwete aliachiwa madaraka ya urais na vizazi vya juu
yake, kwa hiyo na yeye lazima aachie madaraka kwa vizazi vya chini yake
kwa mtindo wa kupokezana vijiti, kwa hiyo wa chini yake si mwingine bali
ni mimi,” alisema January.
Kuhusu matatizo ya Ruvuma, alisema kama akiteuliwa na CCM kugombea
urais kisha akashinda urais atayashughulikia, mathalani ndani ya miaka
mitano atahakikisha mkoa huo unaunganishwa katika Gridi ya Taifa na
kuondokana na matatizo ya mgawo wa umeme.
“Nimekuja Ruvuma kwa kutumia basi ili nijifunze zaidi matatizo ya
hapa, pia najua Ruvuma kuna mgawo mkubwa wa umeme kutokana na
kutounganishwa katika Gridi ya Taifa, nitahakikisha mnaunganishwa ili
muondokane na kero hiyo.
“Pia nitahakikisha hospitali ya mkoa inapanuliwa ili iweze kuhudumia
wagonjwa wengi zaidi na nitahakikisha matatizo ya wakulima yanatatuliwa,
mfano mkulima wa mahindi akienda kuuza mazao yake inabidi alipwe fedha
zake hapo hapo na siyo kusubiri siku nyingine,” alisema January.
No comments:
Post a Comment