WANACCM na baadhi ya wanawake wa Manispaa ya Mtwara Mikindani wamedai
licha ya kuwapo viwanda vingi vinavyoendelea kuzinduliwa katika
manispaa yao, lakini hawapewi ajira kwa madai hawajui lugha ya
Kiingereza.
Wakazi hao walitoa kilio chao jana katika Ofisi ya CCM Mtwara Mjini,
mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi Maalumu, Profesa Mark
Mwandosya, mara baada ya kumaliza kazi ya kutafuta wadhamini wa chama
chake, ikiwa ni sehemu ya kutimiza masharti ya kuwania urais ndani ya
chama hicho.
Wananchi hao wa Mtwara walitoa kilio hicho baada ya Profesa Mwandosya
kuwapa nafasi kueleza yanayowasibu moyoni ili atakapopata nafasi ya
kuingia Ikulu aweze kuyatatua kwa haraka matatizo yao.
“Sisi viongozi tunafikiri tuna hekima na busara na kila tunachosema
tunafikiri tunawawakilisha, hivyo si hekima, busara mnayo ninyi wananchi
na sasa ningependa kusikia kutoka kwenu nini niwafanyie nikifika
Ikulu?” alisema Profesa Mwandosya, ambaye ameendelea kuchanja mbuga
katika mikoa ya Mtwara na Lindi akitafuta wadhamini.
Mara baada ya kupewa nafasi hiyo, alisimama mmoja wa wanachama wa
CCM, Mwamvua Nalinga, aliyesema anawawakilisha wanawake wenzake,
akilalamika wananchi wengi kukosa ajira viwandani kwa madai hawajui
Kiingereza, licha ya kuwa na ujuzi.
“Tunaomba, hapa kuna kampuni kibao, lakini ukienda kuomba kazi unafanyiwa interview (usaili), kwa Kiingereza na sisi hatujui.
“Mfano mimi ni fundi makenika, nina ujuzi na uwezo wa kazi, lakini
sipati kazi sijui lugha, lakini yule anayeajiriwa ambaye anajua
Kiingereza hana ujuzi wala uwezo wa kazi,” alisema Mwamvua.
Mwananchi mwingine alikuwa ni kijana Alli Matunda, ambaye alimtaka
Profesa Mwandosya atakapoingia Ikulu kuweka mwongozo ili kuwafanya
wafungwa wanaoingia na kutoka gerezani kuyapenda maisha yao na si yale
ya gerezani.
Ferdinand Mahendeka, alisema licha ya kuwapo kwa Hospitali ya Rufaa
mkoani Mtwara, lakini bado haiwasaidii wananchi, kwani hakuna dawa,
vifaa pamoja na matibabu kuwa duni.
“Zahanati ya Likombe imepewa hadhi ya kuwa Hospitali ya Wilaya,
lakini haina wodi, madaktari, vifaa tiba na hakuna dawa, tunaomba
ukipata nafasi kwenda Ikulu tuboreshee hilo,” alisisitiza.
Naye Hassan Daima alimwambia Profesa Mwandosya kuwa ahadi ni deni,
kwani wananchi wa Mtwara wameahidiwa sana, lakini hakuna kinachofanyika
na kumtaka kutimiza ahadi alizowaahidi pindi akiwa Rais.
“Ahadi ni deni, Mtwara tuliahidiwa mambo mengi, lakini hakuna, ahadi
zako naomba uzitimize ili na sisi tujisikie vizuri,” alisisitiza.
Akijibu hoja hizo, Profesa Mwandosya alisema amerekodi vilio vyote
vya wakazi wa Mtwara na kusisitiza amezingatia na atavifanyia kazi.
Awali akizungumza na wanaCCM waliofika kumdhamini, Profesa Mwandosya
alisema ana uhakika Oktoba mwaka huu mambo yatakuwwa mazuri kwake.
Aliwashukuru wana CCM wote waliojitokeza kumdhamini, licha ya idadi
ya waliojitokeza kuongezeka ikilinganishwa na idadi iliyowekwa na chama.
“Mmenidhamini pengine wengine ni mara yenu ya pili na wengine
hamjapata kuniona, mmeniona na kunisikia kwenye magazeti, nitawalipa
imani kama mlivyoniamini.
Profesa Mwandosya aliwasili mkoani hapa jana asubuhi saa 05:11 na
kupokelewa na Katibu wa Vijana wa CCM, Joyce Mwenda pamoja na wanachama
wa CCM waliobeba vipeperushi vilivyosomeka “Profesa Mwandosya, Tanzania
Mzalendo Kwanza, Uzalendo wako ndiyo silaha inayokupeleka Ikulu, Mtwara
tunakuamini, tunakuhitaji”.
No comments:
Post a Comment