Mwanasiasa mkongwe na kada wa CCM, Kingunge Ngombare Mwiru (Pichani) amesema anahisi kuna mchezo mchafu unapangwa kwenye mchakato wa kupata mgombea wa urais wa chama hicho tawala, akitaja idadi kubwa ya waliojitokeza kuwa ni ishara mbaya.
Mwanasiasa huyo mkongwe aliyefanya kazi na marais
wa awamu zote nne, pia, bila kumtaja jina, alitumia muda mwingi kwenye
hotuba yake kujibu kauli ya makamu mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula
aliyekaririwa akisema kuwa mgombea wa chama hicho hatakiwi kujinadi.
Kingunge, ambaye amejitokeza hadharani kumpigia
debe Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa alionyesha hofu hiyo jana
wakati mbunge huyo wa Monduli alipokuwa akihitimisha kazi ya kusaka
wadhamini mkoani Dar es Salaam kwenye ofisi za CCM Mkwajuni wilayani
Kinondoni.
Hadi sasa, makada waliochukua fomu kuwania urais
kwa tiketi ya CCM ni 41 baada ya mwanachama mmoja kuchukua fomu jana
akisema atamudu kupata wadhamini kwa njia ya mtandao katika siku tano
zilizosalia. Akizungumza katika mkutano wa kusaka wadhamini ulioandaliwa
kwa ajili ya Lowassa wilayani Kinondoni jana, Kingunge alipingana na
kauli ya Mangula kuwa mgombea wa CCM atanadiwa na chama, si kujinadi
mwenyewe akisema chama hicho kinataka mgombea anayekubalika ndani na
nje.
Siku tatu zilizopita, Mangula alihojiwa na kituo
cha televisheni cha Shirika la Utangazaji Tanzania(TBC) na kusema
mgombea wa chama hicho hatakiwi kujinadi mwenyewe, kusisitiza kuwa
anatakiwa kunadiwa na chama.
Lakini Kingunge aliikosoa kauli hiyo jana akisema
chama hicho kimeweka utaratibu na hakuna sababu ya kuuacha na kuanza
kuwahukumu wagombea kabla ya vikao na kusisitiza kuwa CCM haikuwahi
kuwahukumu wagombea kabla katika chaguzi zilizopita.
“Mchakato ufuate taratibu zilizowekwa,” alisema
Kingunge ambaye aliibuka Kinondoni ambako Lowassa alimalizia shughuli
zake jijini Dar es Salaam.
“Nimemsikia kiongozi wetu mmoja tena juzi juzi
hapa, nikamuona kwenye televisheni anasema mtu hawezi kwenda kujinadi
yeye binafsi, ananadiwa na chama.
“Nikasema eh! hilo hilo. Lakini nataka nimweleze
yeye na wenye fikra kama hizo kuwa kuna ngazi mbili katika utaratibu
wetu; kwanza, mwanachama anayetaka kuwania ubunge, udiwani, urais lazima
ajinadi ndani ya chama, ndivyo tulivyofanya miaka yote kwa mujibu wa
katiba na taratibu zetu. Ndivyo wanavyofanya sasa wakina Lowassa.”
Alisema pili, wagombea wakishajinadi chama kitamteua mmoja ambaye kitamnadi na yeye ataendelea kujinadi.
“Si vizuri watu ambao tumewapa vyeo katika chama
wakaanza ama wakaendelea kukitumia chama chetu kwa mambo yao binafsi.
Kama wana mashaka tupo tunaojua mambo ya chama,” alisema Kingunge huku
akishangiliwa na mamia ya watu.
Kingunge alisema mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya
Kikwete akiwa Dodoma alisema chama kinatafuta mgombea anayekubalika
ndani na nje ya chama hicho ili kuweza kushindana na vyama vingine
No comments:
Post a Comment