Watu
wasiojulikana usiku wa kuamkia jana, waliiba mashine moja inayotumika
kwa ajili ya kuandikishia vitambulisho katika daftari la kudumu la
wapiga kura (BVR) katika kata ya Kayenze wilayani Magu mkoa wa Mwanza.
Akizungumza na mwandishi wetu, kamanda wa polisi wa mkoa wa Mwanza,
Charles Mkumbo, amesema mashine hiyo pamoja na nyingine 13, zilienda
kuchajiwa katika nyumba ya kulala wageni ya BM Lodgei, lakini asubuhi
zilipofuatwa haikuweza kupatikana.
Kamanda Mkumbo amesema baada ya kupata taarifa ya kuibiwa mashine
hiyo, msako mkali ulifanyika ukiwamo wa kuwahoji wasimamizi wa mashine
hizo.
Anasema baada ya kufanyika msako mkali kwa kuweka vizuizi sehemu
mbalimbali, walifanikiwa kuikuta ikiwa imetelekezwa njiani ikiwa salama
bila kuharibiwa, lakini hakuna mtu aliyeweza kukamatwa.
Hata hivyo, kamanda Mkumbo amesema polisi wamefanikiwa kuwashikilia
watu wawili wa nyumba hiyo ya kulala wageni kwa mahojiano ili kufahamu
mashine hiyo ilivyoweza kutoweka katika mazingira ya kutatanisha.
Aidha, ametoa wito kwa waandikishaji kuwa makini pale wanapohifadhi
mashine hizo ili zisiweze kuharibiwa ama kuibiwa na watu wengine.
No comments:
Post a Comment