Dar es Salaam. Siku moja baada ya kuahirishwa
kwa mdahalo wa waliotangaza nia katika nafasi ya urais CCM, imebainika
kuwa viongozi hao wangepaswa kujibu maswali magumu manane yanayohusu
uchumi, utawala bora na utawala wa sheria. Hata hivyo mgombea Balozi
Amina Salum Ali pekee ndiye aliyejitokeza.
Baadhi ya wagombea waliokuwa wametajwa kuhudhuria
mdahalo huo wa moja kwa moja kupitia televisheni ni Naibu Waziri wa
Fedha, Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba, Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye na
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Waziri wa Uchukuzi,
Samuel Sitta.
Akizungumzia utaratibu wa mdahalo huo ulioandaliwa
na Umoja wa Maofisa Watendaji Wakuu wa Kampuni Binafsi nchini ( CEOrt),
Mwenyekiti wake Ali Mufuruki alisema, kila mtangaza nia alitakiwa
kujibu maswali manne ya uchumi na manne ya utawala bora na utawala wa
sheria na ya aina moja.
Maswali ya uchumi waliyotakiwa kujibu ni namna
gani mgombea anaweza kupunguza ongezeko la vijana kukosa ajira, umaskini
na uvunjifu wa amani.
La pili lilikuwa, ‘Ukitilia maanani kwamba sekta
ya kilimo ndiyo tegemeo kuu la maisha kwa asilimia 80 ya Watanzania pia
ina uwezo wa kipekee wa kubadilisha uchumi, ni hatua gani utachukua kama
utateuliwa kuwa rais?’
La tatu liliuliza, ‘je, kama ukiteuliwa kuwa rais
utafanya nini kuhakikisha uchumi wetu unakua na manufaa yake yanakuwa
shirikishi na tofauti kati ya maskini na matajiri haiwi kubwa kiasi cha
kuhatarisha amani katika nchi yetu?’
Jingine lilipaswa kuulizwa, Ukiwa kiongozi
atakayekuwa ofisini wakati huu wa uwekezaji katika sekta ya gesi asilia,
utachukua hatua gani kuhakikisha matumaini ya utajiri na maisha bora
waliyonayo Watanzania kwa sekta hii yanatimia?’
Watangaza nia hao walitakiwa kueleza pia iwapo
wanakubali kwamba Tanzania haiwezi kufikia malengo yake ya maendeleo
bila kuwekeza katika miundombinu. ‘Kama unakubali, utatumia mbinu
gani kupata fedha hizo nyingi zinazotakiwa katika kuwekezaji kwenye
miundombinu?’
Kwa upande wa utawala bora na utawala wa sheria,
walitakiwa kueleza ni vipi watachukua hatua kuhakikisha usimamizi mbovu
wa masilahi ya nchi, rushwa na upuuzwaji wa sheria unadhibitiwa.
Pia, walitakiwa kueleza watachukua hatua gani
kuhakikisha ujangili unatokomezwa nchini, watakomeshaje upotevu mkubwa
wa mapato unaotokana na ukwepaji kodi na watatumia njia gani kuhakikisha
mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yanakomeshwa.
Hata hivyo, Mufuruki alisema kuwa hadi kufikia
juzi mchana watangazania watatu pekee ndiyo walikuwa wamethibitisha
ushiriki wao na baadaye Sumaye na Nyalandu wakitoa udhuru.
Watangaza nia wengine, walionekana kuomba radhi
kupitia mitandao ya kijamii wakidai kuvurugwa na ratiba ya mdahalo huo
ambao awali walielezwa ungefanyika asubuhi kabla ya kuahirishwa.
No comments:
Post a Comment