Profesa Mwandosya akosoa mfumo wa uchaguzi CCM

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjf3h6TlZfepoLVUaPsbA975LkPeZQSJsL9iCkqYOegqXy6rCBHYtPa75Qg9bHuDeIHBZUJf6tOli13jvqUWD9EU6a3KdXcieaoSW_FQpeLBHz8DA9_1f9UY3mCAoPpT0fIikbKnReHpKsv/s1600/DSC_0129.jpgDar/Mikoani. Makada wa CCM wanaoendelea kusaka wadhamini mikoani wamekuwa wakitoa kauli tofauti, ikiwamo wito uliotolewa na Profesa Mark Mwandosya kuitaka CCM ibadili mfumo wake wa uchaguzi ili apatikane kwanza mwenyekiti wa chama hicho tawala, kabla ya mgombea urais.
Wengine waliotoa kauli jana ni Amina Salum Ali ambaye amewaponda wanaoamini kuwa wanawake hawawezi kuwa viongozi, Samuel Sitta aliyesisitiza kutaifisha mali za mafisadi na Steven Wasira ambaye amelia kuchezewa rafu ili aenguliwe kwenye kinyang’anyiro.
Ushauri wa Mwandosya
Profesa Mwandosya alisema utaratibu wa kuanza kumchagua mgombea wa kiti cha urais kabla ya mwenyekiti wa chama ni mbovu na ndiyo unaosababisha msururu wa watu kutaka kuwania nafasi hiyo ya juu serikalini.
“Kwa maoni yangu tungeanza kwanza kumpata mwenyekiti wa chama, kabla ya mgombea urais na hii ingesaidia kupunguza idadi ya makada wa CCM wanaotaka kuwania urais. Idadi ya watu 30 walijitokeza kutangaza nia ingepungua sana, lakini sasa hatuwezi kuvuruga utaratibu uliopo,” alisema alipowasili mkoani Geita kutafuta wadhamini. Profesa Mwandosya aliyekuwa ameongozana na mkewe na mtoto wake mkubwa, Max na Katibu wa Siasa na Uenezi Mkoa wa Mbeya, Bashiru Madodi aliwasili mkoani Geita saa tano asubuhi akitokea mkoani Mwanza.
Wanawake wanaweza
Amina ambaye kwa sasa ni Balozi wa Umoja wa Afrika (AU) alisema watu wanaowabeza wanawake kugombea uongozi kwa madai kuwa hawawezi, wana mawazo mepesi na kusahau kuwa wapo wengi walioongoza mataifa makubwa na wengine ambao bado wanashikilia nafasi za juu katika nchi zao.
Alitaja nchi ambazo kuna viongozi wa juu wanawake kuwa ni Liberia na Ujerumani na kukumbushia michango ya wanawake kama Benazir Butto, Margareth Thatcher na Indira Gandi.
Alisema Mwanamke ndiye anayeguswa na matatizo mbalimbali katika jamii, ikiwamo ya afya, umaskini, elimu na usimamizi wa familia, kwa vile ndiyo anayokabiliana nayo mara kwa mara katika maisha ya kila siku ya Watanzania.
“Dhana ya mwanamke hafai kuongoza taifa, imepitwa na wakati na inabidi wanaopinga warudi kwenye historia na kupekua kumbukumbu za viongozi wanawake waliopata mafanikio wakati wakiziongoza nchi zao,” alisema.
Sitta kutaifisha mali za mafisadi
Akizungumza muda mfupi baada ya kukamilisha ziara yake ya kuzuru kaburi la aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Omar Ali Juma katika Kijiji cha Wawi, Mkoa wa Kusini Pemba, akiwa ameambatana na wana-CCM kadhaa, Sitta ambaye ni Waziri wa Uchukuzi aliapa kutaifisha mali za viongozi wote zilizopatikana kwa njia haramu na kuhujumu uchumi, iwapo chama chake kitamteua kuwa mgombea urais. “Kama nikijaliwa kufika katika safari yangu, sheria moja kali itakuwapo, kwamba kiongozi mwenye mali isiyoelezeka, basi kwa kiwango kilekile tutaitaifisha,” alisema Sitta.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved