WAZIRI wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ambaye
pia anaomba CCM impitishe kuwa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu
baadaye mwaka huu, Bernard Membe amekiri kwamba katika kinyang’anyiro
cha urais ndani CCM, mtu anayemnyima usingizi ni Waziri Mkuu Mizengo
Pinda.
Akizungumza na wanachama waliojitokeza kumdhamini jana, Membe alisema
Pinda asingechukua fomu ya urais ndani ya CCM, angefurahia ushindi tu
na tayari angekuwa ameshona suti na kushangilia ushindi.
Alisema kuwa Waziri Mkuu Pinda ni mchapakazi, asiye mbinafsi,
mwadilifu, mvumilivu sana mwenye hekima na busara ya hali juu,
mwanasheria aliyebobea na ndiye mwalimu aliyemfundisha kazi.
“Wengine wote hawanitishi nitawagonga lakini nikifika kwa Pinda
itabidi nipumue kwanza...kwa hiyo mimi na Pinda ni pacha nikishindwa
mimi nitamuunga mkono lakini akishindwa naamini ataniunga mkono, ndio
maana hata wakati nakuja huku nimewasiliana naye akanieleza nenda na
amenisaidia nimepata wadhamini wa kutosha,” alisema.
Membe amesema kuwa Mungu akimjaalia kuteuliwa na CCM kushinda urais
atahakikisha baadhi ya miradi inayotumia fedha za ndani ambayo inasuasua
ikiwemo ujenzi wa barabara ya Sumbawanga hadi Mpanda unakamilika,
lakini pia bonde la Ziwa Rukwa linatumika kuzalisha chakula ambacho
kitalisha nchi nzima kwa kuwa ardhi yake ina rutuba na inafaa kwa
kilimo.
Pia, Membe aliwaasa baadhi ya wanaCCM kuacha kuwashangilia kila
mgombea anayepita kuomba udhamini kwa kuwa si wote wana sifa kwani wenye
sifa stahiki ni yeye na Waziri Mkuu Pinda.
Awali, Katibu Mwenezi wa Mkoa huo, Clement Bakali alisema kuwa
mgombea huyo amepata wadhamini 855 kutoka wilaya zote za mkoa wa Rukwa.
No comments:
Post a Comment