CHAMA cha NCCR - Mageuzi kimesema hakitajitoa katika kundi la Umoja
wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kwa vile lengo lake si mgawanyo wa
madaraka bali Katiba.
Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia alisema hayo jana wakati
akitoa Maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho iliyokaa jana na kusema
wamedhamiria kutotoka katika kundi hilo na kwamba watavuka salama katika
mgawanyo huo wa madaraka.
Alisema Ukawa ni zao lao, hivyo hawatatoka wala kuvunjika kama
wanavyodaiwa na baadhi ya watu na kutaka vyama vingine kuendelea
kuaminiana kwa kuwa NCCR ipo kwa moyo thabiti.
“Kikao chetu tumeazimia kwa malengo ya chama yatafikiwa ndani ya
Ukawa kwani si lengo letu katika kugawa madaraka bali ni Katiba kwanza
kwa kusimamia mawazo ya wananchi hivyo kwa umoja vyama vitahakikisha
vinapigania mawazo ya Watanzania,” alisisitiza.
Alisema katika mgawanyo wa madaraka vyama hivyo vyenye lengo moja
vitahakikisha vinavuka salama kwa kugawana vizuri kwa maelewano na jambo
la msingi ni kuaminiana kwani hakuna linaloshindikana.
Akizungumzia Katiba pendekezwa, alidai kuwa kwa mujibu wa Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba imefutika na imetupwa kwani hakuna mwenye uwezo wa
kuitisha Kura ya Maoni tena hivyo serikali kushindwa kuwapatia Katiba
mpya wananchi licha ya kutoa mawazo yao.
Kuhusu uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura alisema
linaweza kusababisha vurugu wakati wa kuwekwa wazi huku kampeni zimeanza
hivyo hatua zichukuliwe kudhibiti hali hiyo ikiwepo kujiandikisha mara
mbili kutokana na kuwa mpaka sasa watu 5,000 wamegundulika kujiandikisha
mara mbili.
No comments:
Post a Comment